Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ametoa kiasi cha shilingi Milioni tano kama msaada baada ya kuguswa na hali ya mtoto, Latifa Ibrahimu ambaye hawezi kutembea wala kukaa.
Akikabidhi msaada huo kwa familia ya Bi Rehema Kadogosa ambaye ni mamam mzazi wa mtoto huyo, mkazi wa Mwenge Mlalakuwa jijini Dar es Salaam, Kwa niaba ya Rais Magufuli Katibu wa Rais, Ngussa Samike amesema Rais ametoa msaada huo baada ya kuguswa na hali ya mtoto na kuwataka wakina baba kutokimbia majukumu yao anapozaliwa mtoto mwenye ulemavu ndani ya familia.
Akipokea msaada huo mama mzazi wa mtoto huyo, Bi Rehema amemshukuru Rais Magufuli kwa namna anavyowasaidia Watanzania hasa wananchi wanyonge wasiojiweza.
Kwa yeyote ambaye ataguswa kutoa msaada zaidi kwa mtoto Latifa anaweza kuwasiliana na mzazi wa mtoto huyo kupitia namba za simu 0713 323 305 au kuwasilisha mchango wake kupitia akaunti namba 0152337759200 kupitia Benki ya CRDB tawi la Mikocheni jijini Dar es Salaam.