Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto aliyeibuliwa na Mwananchi akiwa hoi arejewa na tabasamu

Video Archive
Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatimaye afya ya mtoto, Said Shaban (10) aliyekuwa taabani kitandani kwa kukosa matibabu baada ya kuungua moto kisha miguu yake kupooza kwa zaidi ya mwaka mmoja, imeanza kuimarika.

Said anaendelea kupatiwa matibabu maalum katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya waziri wa afya, Ummy Mwalimu kuagiza asaidiwe.

Februari Mosi mwaka huu Mwananchi lilichapisha habari ya mtoto Said akiomba msaada wa matibabu baada ya bibi yake kushindwa kumpeleka hospitali kutokana na hali ya uchumi kuwa ngumu.

Said alikata tamaa ya kuishi na mara kadhaa aliomba rafiki zake wamnunulie sumu ya panya akiamini kifo kingekuwa suluhisho la mateso hayo.

Gazeti hili lilimtembelea mtoto huyo katika wodi ya watoto na kumkuta akiwa ameketi kitandani huku akitabasamu tofauti kabisa na hali aliyokuwa nayo awali kabla ya matibabu kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kukaa, kusimama wala kutembea zaidi ya kulala. Daktari wa watoto wa MNH, Farhia Ally alisema kwa sasa afya ya Said inaendelea kuimarika na anapatiwa matibabu. “Utapiamlo ulimfanya akonde kupita kiasi hivyo anapatiwa matibabu na lishe na anaendelea vizuri kabisa,” alisema.

Bibi yake Said, Julieth Simkanga aliishukuru MNH akisema hakutarajia kama siku moja mjukuu wake angepata nafuu kutokana na mateso makali aliyokuwa akipitia. “Naishukuru hospitali hii kwa kumtibu mjukuu wangu bure kabisa, hapa tulipo tunakula na tunalala bure wala hatudaiwi chochote kile, nalishukuru gazeti la Mwananchi kwa kuja kutufichua, mlipotuandika Serikali ilikuja kutusaidia, mjukuu wangu leo anatabasabu ningefanya nini mimi,” alisema.

Ofisa uhusiano wa MNH, John Stephen alisema Said anapewa mahitaji muhimu bila gharama na matibabu yote yanafanywa chini ya mkurugenzi wa huduma za upasuaji, Baruan Sufian. Bibi wa mtoto huyo amewaomba wasamaria wema kumsaidia kupitia namba 0710319128 kutokana na hali duni.

Soma zaidi: Serikali yamsaidia mtoto aliyetaka kujiua kwa sumu



Chanzo: mwananchi.co.tz