Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto aeleza maisha ya Anna Mghwira

04a4e3cb6cc391256999935e9c30e9b9 Mtoto aeleza maisha ya Anna Mghwira

Mon, 26 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MTOTO aliyelelewa na Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Anna Mghwira, ameelezea maisha ya kiongozi huyo alivyokuwa mcha Mungu, mwimbaji na mwenye ndoto ya kuendelea na siasa kwa lengo la kuwatumikia wananchi hata baaada ya kustaafu.

Hellen Mghwira, ambaye ni mtoto wa kaka yake mkuu huyo wa mkoa aliyefariki juzi, alisema jambo kubwa alilowaachia ni kuwafundisha kujitegemea, kumpenda Mungu na kufanya kazi kwa bidii kuondoa utegemezi katika maisha.

“Karama aliyokuwa nayo ambayo watu hawakuijua sana ni uimbaji, alikuwa akiimba sana kanisani na nyumbani, kabla ya kuanza kuumwa alikuwa akiimba na kucheza sana nyimbo za Injili,” alisema.

Alisema alikuwa na ndoto ya kuendelea na siasa, kuwatumikia wananchi na hata alipostaafu, aliendelea kuwasaidia watu walioomba msaada wake.

Kwa mujibu wa Hellen, Mghwira alipenda nyimbo za Injili hasa za mwimbaji Christina Shusho na zaidi wimbo wa “Nipe Macho Nione”.

Alisema shangazi yake huyo ambaye hata hivyo alimtaka awe anamuita ‘Mama’, alikuwa na uwezo wa kusoma Biblia Takatifu na kuitafsiri kwa kina.

Akielezea malezi waliyopewa, alisema: “Hakupenda neno kuchoka na ukimwambia umechoka atakwambia hapana fanya kazi.

Malezi yake ametuachia kitu kikubwa sana, cha kujitegemea, hakupenda kututengenezea njia ya kupewa tu moja kwa moja, bali alitaka kuona juhudi za mtu ili akusaidie unapokwama.”

Vile vile alisema Mghwira alikuwa mtu wa kutunza mazingira na alipenda maua. Alipenda pia kusoma vitabu kiasi kwamba, mtu akiingia anapokelewa na wingi wa vitabu kama mapambo.

Kuhusu ugonjwa, Hellen alisema, Mghwira alianza kusema mapema kwamba anajisikia vibaya na baada ya siku kadhaa alipiga simu kwa watu akisema anajisikia kuumwa.

Alisema kabla ya kulazwa, alimpigia mtu simu (hakumjua jina) katika ofisi yake ya zamani (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa) akamweleza kuwa anaumwa na huyo mtu akamshauri aende hospitali.

“Hospitali waligundua kuwa ana tatizo la nimonia na baadaye madaktari walisema ana tatizo la kupumua. Kifo chake kimeleta mshituko mkubwa sana kwetu familia, lakini kazi ya Mungu haina makosa,” alisema Hellen.

Mghwira alifariki Alhamisi iliyopita katika Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha alikokuwa amelazwa kwa matibabu. Anatarajiwa kuzikwa kesho nyumbani kwake Arumeru, mkoani humo.

Kwa mujibu wa Hellen, Anna Mghwira ameacha watoto watatu ambao mmoja ambaye ni mwanasheria aliyepo nchini Uingereza.

Wawili waliopo nchini, yupo mfanyabiashara na mwingine ni mtaalamu wa masuala ya Tehama.

Chanzo: www.habarileo.co.tz