Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msipige kura kishabiki - Majaliwa

2efd7877f197b1eb7a96bc1d3fbb7746 Msipige kura kishabiki - Majaliwa

Tue, 8 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa alitahadharisha wananchi wasifanye mzaha siku ya kupiga kura, wasimchague mtu kwa sababu ya ushabiki na badala yake wamchague mgombea urais wa CCM, Rais John Magufuli.

Pia, ameomba wawachague wagombea ubunge na udiwani wa CCM ili waweze kushirikiana kuendeleza miradi ya maendeleo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina fedha za kutosha kuwatumikia Watanzania kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya, maji, elimu.

Aliyasema hayo jana alipohutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Soko la Holili Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Katika mkutano huo, alimuombea kura mgombea urais wa CCM, Rais Magufuli, mgombea ubunge Jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda na wagombea udiwani kupitia CCM.

"Tunaomba kura zenu wanaHolili na Watanzania wote kwa Rais Dk Magufuli ili akaendelee kuboreshe maendeleo katika sekta ya elimu itakayotuwezesha kuwa na wataalamu wengi. Nawaomba mumchague Dk Magufuli kwa sababu ameitendea haki nchi yetu na ni kiongozi mcha Mungu na mpenda maendeleo,"alisema.

Akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama inayowakabili wakazi wa Holili, Majaliwa alisema serikali imetoa Sh. bilioni 1.5 kufanya utafiti, kuona namna watakavyoyatoa maji kutoka Ziwa Chala na kuyasambaza kwa wananchi.

Alisema mradi mwingine wa maji unaotekelezwa katika wilaya hiyo ni Mradi wa Maji Njoro II (Tarakea).

"Serikali imekamilisha mradi huu kwa shilingi milioni 200 na unatoa huduma ya maji katika eneo la Tarakea. Malengo ya serikali kwa sasa ni kutafuta fedha ili kuupanua mradi huo na kuweza kutoa maji katika maeneo mengine ya tarafa nzima ya Tarakea"alisema.

Majaliwa alisema mradi wa kijiji cha Ngareni wenye thamani ya Sh milioni 812.4 uliohusisha ujenzi wa tangi la kuhifadhi maji la lita 75,000, ujenzi wa vituo 15 vya kuchota maji na ufungaji mabomba ya njia kuu na njia za kusambaza maji vimekamilika.

Alisema ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wakazi Rombo, serikali Julai mwaka huu ilivunja Kampuni ya Maji ya Kill Water na kuanzisha Mamlaka ya Maji Rombo (ROWASA)

Chanzo: habarileo.co.tz