Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Moi kuanza upasuaji wa mgongo

Video Archive
Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Mifupa (Moi) inajipanga kuanzisha kituo maalumu kitakachotoa huduma za upasuaji wa mgongo baada ya kuwapo wagonjwa wengi wanaofika katika taasisi hiyo wakiwa na tatizo hilo.

Pia, wataalamu wa taasisi hiyo watakwenda kuwapa mafunzo madaktari wa hospitali za wilaya na mikoa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenda Moi kufuata upasuaji wa kawaida.

Mkurugenzi mtendaji wa Moi, Dk Respicios Lwezimula alisema hayo jana katika maadhimisho ya miaka 22 ya taasisi hiyo huku madaktari wakijitolea kufanya upasuaji kwa wagonjwa 11 siku ya mapumziko.

Alisema tayari hatua za awali za uanzishwaji wa kituo hicho zimeanza na mchakato wa kumtafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi utaanza.

“Katika kipindi cha miaka miwili tunajivunia tumefanya kazi kubwa sana, kwa kuwa imani ya Watanzania dhidi ya huduma zetu imekuwa kubwa, wamezidi kumiminika kupata matibabu tumeona kupunguza msongamano tuanzishe kituo kwa ajili ya upasuaji wa migongo, makadirio ni kwamba ujenzi wake hautakuwa chini ya Sh25 bilioni.

“Kana kwamba hiyo haitoshi tunataka tuwafikie madaktari katika hospitali za wilaya na mikoa kuwajengea uwezo ili wafanye upasuaji kule na hilo litatupunguzia mzigo maana kwa sasa tunafanya upasuaji kwa wagonjwa kati ya 500 na 700 kwa mwezi,” alisema Dk Lwezimula.

Alifafanua kuwa Moi inakabiliwa na changamoto ya gharama za vifaa tiba vya kuunganishia mifupa ambavyo vyote vinaagizwa nje ya nchi.

“Asilimia 95 ya wagonjwa wetu wanatakiwa kufanyiwa upasuaji, changamoto ni kwamba huwezi kumwekea mtu chuma chochote lazima utumie chuma maalumu na chenye ubora. Vifaa hivyo tunaagiza nje gharama yake ni kubwa sana, sasa kama inawezekana wataalamu wa hapa nchini walete teknolojia ya kutengeneza hivi vyuma hapa angalau matibabu haya yawe nafuu,” alisema.

Mkurugenzi wa tiba wa taasisi hiyo, Dk Samuel Swai alisema muda si mrefu wataanza kufanya upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu lengo likiwa ni kwenda sawa na mabadiliko ya teknolojia katika upasuaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz