Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameshindwa kuitikia wito aliopewa na Jeshi la Polisi kufika katika Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kinondoni kuhojiwa kuhusu mauaji ya aliyekuwa kada wa chama hicho, Ali Kibao.
Wito wa polisi ulitolewa Septemba 16, 2024 na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (SSP) Davis Msangi, ukimtaka Mnyika kufika ofisini kwake leo Jumatano Septemba 18, 2024 ili kukamilisha uchunguzi, kwani kuna masuala anayoyafahamu.
Akijibu wito huo, Mnyika kupitia kampuni ya uwakili ya Matwiga Law Chambers, amesema hawezi kuitikia wito huo kwa kuwa yuko kwenye vikao vya kamati kuu.
“Mteja wangu anakiri kupokea barua yako ya Septemba 16, 2024 iliyofikishwa kwake Septemba 17, 2024 asubuhi, ikimtaka kufika ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makossa ya jinai mkoa wa kipolisi Kinondoni Septemba 18, 2024 saa nne asubuhi.
“Kwamba, anawajulisha kuwa kama mtendaji mkuu wa chama atakuwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachofanyika hapa Dar es Salaam kwa siku ya tarehe 17 na 18 Sepemba 2024, hivyo atashindwa kufika siku iliyopangwa,” imeeleza sehemu ya barua iliyosaidiwa na wakili Hekima Mwasipu.
Hata hivyo, wakili Mwasipu hakueleza mteja wake Mnyika ataripoti polisi lini.
Taarifa za kuitwa kwa Mnyika zilijulikana tangu Septemba 12, 2024, ambapo wakili huyo alisema waliletewa taarifa na polisi za wito huo.