Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkuyu ulionyongea watu sasa unatoa digrii

Mkuyu Pic1 Mkuyu ulionyongea watu sasa unatoa digrii

Thu, 12 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mji wa Dodoma una historia ya kuvutia kuanzia chimbuko la jina lenyewe hadi simulizi za mti uitwao mkuyu uliotumika kunyongea watu na kuwazika.

Kuna uhusiano mkubwa wa asili ya neno Dodoma na mahala ulipo mti huo ambao kwa sasa kuna Chuo kikuu cha St John, zamani sekondari ya Mazengo.

Eneo hilo linajulikana kwa jina la Kikuyu jina litokanalo na uwepo wa mti huo wa mkuyu. Katika eneo hilo ndipo neno Dodoma lilipopatikana. Ilikuaje?

Inaelezwa kuwa zamani jirani na mti huo kulikuwa na tembo aliyedidimia na kuzama, kwa Kigogo kitendo hicho walikiita idodomya au dodomi yaani kuporomoka au mahali palipodondoka.

Wazungu walipoingia katika mji huo walishindwa kutamka Idodomya, badala yake wakaita Dodoma.

Mti wa mkuyu

Mti wa mkuyu uliotumiwa na wakoloni kwa kunyonga watu mkoani Dodoma ni sehemu ya historia ya ukoloni ambayo inahusiana na dhuluma na ukatili wa wakoloni dhidi ya watu wa Afrika.

Wakati wa ukoloni, hasa wakoloni wa Kijerumani na Waingereza walitumia njia za kikatili kudhibiti na kuwatisha wenyeji.

Mojawapo ya mbinu hizo za kikatili ilikuwa kunyonga watu ambao walionekana kuwa na upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni au walioshutumiwa kwa vitendo vya uhalifu.

Mti huu wa mkuyu ulitumiwa kama chombo cha adhabu ya kunyonga watu hadharani, ili kuwatia hofu wenyeji.

Watu waliokuwa wakipinga ukoloni walikamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma mbalimbali, kisha waliopatikana na hatia, mara nyingi katika mazingira ya ukosefu wa haki, walinyongwa katika mti huu.

Mkuyu, kama mti wenye mizizi mikubwa na matawi mapana, ulionekana kuwa na nguvu ya kiasili na uimara, hivyo kuwa mti unaofaa kwa kunyonga watu.

Mti huu umebaki kama alama ya ukatili wa kikoloni na pia ushahidi wa jinsi wakoloni walivyotumia nguvu na ukatili kudhibiti watu.

Mkuyu huo mkubwa ambao umetanda eneo kubwa takribani mita 20 kila upande kutoka kwenye shina, ni alama inayoonyesha kuwa mahala hapo palitumika kama mahakama ya kidhalimu.

Aidha, kwenye mkuyu huo upo mfano wa kitanzi kilichotumika kunyongea watu walioikosea Serikali ya mkoloni, ambacho kimetengenezwa kwa waya mgumu kama kilivyokuwa kitanzi halisi kilichotumika kwa wakati huo.

Kitanzi halisi ambacho kilitumika kilizama kwenye shina la mkuyu huo baada ya shina lake kukua, hata hivyo alama inayoonyesha kufungwa kitanzi hicho ipo kwenye shina la mkuyu huo mkubwa ambapo ukifika inaonekana bila kujificha.

Kitanzi hicho kinaonyesha ni jinsi gani raia wan chi hii walikufa kwa mateso wakati wakipambana kumwondoa mkoloni.

Mti huo kwa sasa unajulikana kwa jina maarufu ‘mdigrii’ kwa sababu vipo vimbweta ambavyo wanafunzi wa chuo hicho wanavitumia kujisomea na kupata digrii zao chini ya kivuli kizuri cha mkuyu huo mkubwa wenye miaka mingi.

Maelezo ya Mtemi Mazengo

Kitukuu cha Mtemi Mazengo ambaye alikuwa mtawala wa Wagogo enzi za mkoloni, Frank Mazengo, anaeleza eneo hilo lilikuwa ni pori.

Anasema hata miili ya watu walionyongwa ilizikwa kwenye pori hilo ambalo baadaye wamisionari walijenga shule ya sekondari ya Alliance baadaye ikaitwa Shule ya Sekondari Mazengo kabla ya kubadilishwa na kuwa Chuo Kikuu cha St John’s.

“Ili kutunza historia isipotee wakati wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Alliance, mkuyu huu haukuondolewa na hata kitanzi halisi kilipozama kwenye shina la mti, tulilazimika kuweka kitanzi kingine cha mfano kwenye tawi hilo, ili kuonyesha watu kuwa mti huo ulitumika kunyongea babu zetu waliokuwa wakikutwa na hatia mbalimbali ikiwemo ya kuua kwa kukusudia,” anasema Mazengo.

Mtaalam wa teknolojia wa Chuo cha St John’s, Margaritha Chitema amesema mkuyu huo kwa sasa unajulikana kwa jina maarufu la mdigrii kwa sababu ndipo wanafunzi wanaosoma chuoni hapo wanapata elimu yao kwa kuwa ni eneo la kujisomea.

Amesema chuo hicho kimeunganisha mtandao wa intaneti kwenye vimbweta vilivyopo kwenye mti huo pamoja na taa za umeme ili kuwawezesha wanafunzi kujisomea wakati wote mchana na usiku.

“Wanafunzi wengi hawajui historia ya huu mti na kwa sababu wamekuja kusoma ili wapate digrii zao wameubatiza huu mti kwa jina la mdigrii, hivyo kuondoa kabisa historia mbaya ya mti huu na ndiyo maana huwa wanasoma muda wote bila kuogopa,” anasema Margaritha.

Je, wajua

Chimbuko la jina Dodoma ni tembo aliyedidimia eneo la Kikuyu. Kitendo hicho kwa lugha ya Kigogo kinajulikana kama ‘idodomya’.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live