Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mjadala bajeti ya Serikali bado ni wa moto

Mbunge Mtaturu Aibana Serikali Ujenzi Wa Barabara Mjadala bajeti ya Serikali bado ni wa moto

Thu, 22 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wabunge wameitaka Serikali iangalie vyanzo vingine vya mapato badala ya nyongeza ya Sh100 kwenye petroli na dizeli pamoja na Sh1,000 katika mfuko wa saruji kwa kuwa litaongeza gharama ya maisha kwa wananchi.

Wabunge wanaendelea na mjadala wa bajeti ya mwaka 2023/24 ya Sh44.4 trilioni iliyowasilishwa bungeni Juni 16, mwaka huu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Akichangia hoja hiyo bungeni jijini Dodoma jana, Mbunge wa viti maalumu, Kunti Majala alisema tozo ya Sh100 kwenye petroli na dizeli kama itaachwa hivyo, itachangia mfumuko wa bei.

Majala alisema miezi ya nyuma, Serikali iliamua kuweka ruzuku kwenye mafuta hayo kutokana na wimbi la vita vya Ukraine na Russia.

“Waziri umetuletea ongezeko la tozo ya Sh100, ni dhahiri unapoongeza kodi unapandisha nauli za usafiri na gharama za vyakula, nataka tutumie vyanzo vingine vya mapato badala ya kwenda kwenye mafuta,” alisema mbunge huyo.

Kuhusu kodi ya Sh1,000 kwenye mfuko wa saruji, Majala alisema ujenzi ni gharama kubwa, hususani vifaa, hivyo alishauri bei ipunguzwe kama ilivyofanyika kwenye tozo za mafuta ili wananchi wapate nafuu pindi wanapojenga nyumba bora za makazi na biashara.

Mbunge wa Maswa Magharibi (CCM), Mashimba Ndaki, alishauri Serikali kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wakulima pindi bei za mazao yao zinapoporomoka.

“Sio geni, ni wazo linalofanywa na nchi zilizoendelea na sehemu nyingine sisi tunaweza kufanya hivyo kwa kuwatoza wakulima pindi zinapokuwa ziko juu, lakini pia ruzuku ili kufidia bei zinapoanguka,” alisema Mashimba, aliyewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Kuhusu mifumo ya kodi, Mbunge wa Segerea (CCM), Bonnah Kamoli alisema Serikali irekebishe mifumo ya malipo katika halmashauri kwa kuwa haifanyi kazi kwa mwezi mmoja sasa, hali inayochagia upotevu wa fedha za maendeleo zinazotengwa na Serikali.

Naye Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk Pius Chaya aliitaka Serikali kuboresha mfumo kukusanya mapato kwenye halmashauri nchini kwa sababu umekuwa na changamoto nyingi, ikiwamo ya kutoa kumbukumbu namba ya malipo tofauti na kiasi cha fedha halisi kinachotakiwa.

“Mfano kwenye jimbo langu la Manyoni, kuna wakati mkusanyaji mapato hukusanya Sh5 milioni, anaenda nazo mkononi anatolewa kumbukumbu namba yenye thamani ya Sh1 milioni, hii inamaanisha kuwa hapo tayari kuna harufu ya wizi,” alisema.

Katiba mpya

Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khenani aliiomba Serikali kuhakikisha kuwa Sh5 bilioni zilizotengwa kwenye bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya mchakato wa Katiba mpya zinatolewa ili uanze mapema.

“Naona katika hotuba yako mmetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya Katiba mpya, nawashukuru sana kwa sababu mmetenga, lakini katika Serikali yetu kutenga ni jambo moja na kupeleka fedha ni jambo jingine, tunaomba fedha hiyo iende,” alisema.

Alimuomba Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kupeleka fedha kwa ajili ya mchakato huo uanze na uzingatie maoni na ushauri wa Watanzania ili yatakayopitishwa yatekelezeke.

Pia alisema tozo zilizopo kwenye miamala ya simu kukatwa mara mbili ni kero kwa wananchi wa kipato cha chini. “Tumeona hapa mnavyokwenda kusaidia kuondoa makato kwa yule anayetuma…tunajua huyu anayetuma si mfanyabiashara, kwani tulisajili ya nini, kwa hiyo mwongozo utolewe, vinginevyo mnatengeneza gharama isiyo na sababu,” alisema.

Alisema mtu anakatwa kwenye simbaking lakini anakatwa tena benki na kuhoji kwa nini Serikali isikae na kampuni za simu angalau makato yawe ya aina moja.

Zawadi wanaodai risiti

Mbunge wa Busega (CCM), Simon Songe alishauri Serikali kuanzisha mfumo wa kumpongeza mwananchi anayedai risiti anapokwenda kununua bidhaa ili kuwapa motisha na kuiongezea Serikali mapato yanayopotea kutokana na wafanyabiashara kutoingiza mauzo kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alitoa mfano kwa mtu aliyefanya manunuzi ya Sh3 milioni mwisho wa mwezi akapata faida ya Sh50,000, atajua kuwa anapoomba risiti mwisho wa mwezi atapata faida kupitia simu yake.

“Ninaamini mapato ambayo tunayapoteza kwa wananchi kutokudai risiti ni makubwa kuliko mapato ambayo tutatumia kumpa mwananchi atakayeomba risiti,” alisema.

Wakati huo huo, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amewaagiza mameneja wa mifuko ya hifadhi jamii kuwasilisha kwake majina ya waajiri sugu wanaodaiwa michango ya wafanyakazi wao ndani ya siku saba kuanzia jana.

Aliagiza pia ikakamilishe zoezi la kusaini mikataba ya kulipa madeni ya michango ya wanachama kabla ya Juni 30, 2023.

Agizo hilo limekuja baada ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuomba waajiri wanaoshindwa kupeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii kuchukuliwa hatua kwa kuwa wanasababisha kero kwa wastaafu na wanachama husika.

Akizungumza jana akiongozana na wawakilishi wa Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Shirika la Hifadhi ya Jamii, Katambi aliagiza mifuko hiyo kuhakikisha kuwa inawalipa wanachama ndani ya siku 60 za kisheria wanachama ambao nyaraka zao zimewasilishwa kwa ukamilifu.

“Mameneja wahakikishe kuwa hakuna malalamiko ya wanacham akatika mikoa wanayoiongoza na kuhakikisha kuwa waajiri wote wanalipa na kuwasilisha madeni ya michango ya watumishi wao kila mwezi,”alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: