Moshi. Serikali imeanza kufuatilia upotevu wa zaidi ya Sh5 bilioni za benki ya KCBL ulioifanya iyumbe kiuchumi hata kunusurika kufungwa na Benki Kuu kwa kutokidhi mtaji wa kujiendesha.
Ufuatiliaji huo umetangazwa na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira leo Ijumaa Agosti 31, 2018 kwenye mkutano mkuu wa wanahisa wa benki hiyo ambao wamependekeza iondolewe mikononi mwa ushirika na kuwa kampuni ili ijiendeshe kibiashara.
Mghwira amesema anasikitishwa na baadhi ya wafanyakazi kujimilikisha benki hiyo na kuifanya kama maduka binafsi hivyo kujichotea fedha kinyume na utaratibu.
“Ni kitu cha ajabu sana kuona mkoa huu wenye vyama vingi vya ushirika vinakufa ilhali wataalamu wapo, viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza vyama vya ushirika pamoja na benki za ushirika wamefanya vyama hivyo kama vyao,” amesema.
Kutokana na matumizi mabaya ya fedha, amesema baadhi ya viongozi wa chama kikuu cha ushirika (KNCU) wamekamatwa kwa ubadhirifu wa fedha za chama hicho.
Amesema anasikitishwa kwani licha ya mkoa huo kuwa na chuo kikuu na vyama vya ushirika, sekta hiyo inakufa wakati wataalamu wapo.
Aidha, Mghwira amesema benki hiyo ilipoanza kuyumba alisimama kidete kuitetea isiuzwe.
Pamoja na hayo yote, amewataka wajumbe na viongozi wa benki hiyo kuanza historia mpya bila kupoteza jambo lolote baada ya benki hiyo kubadilishwa kama kampuni ili iendeshwe kibiashara zaidi.