Kilimanjaro. Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amemtaka Kamanda wa Polisi mkoani humo kumchukulia hatua za kinidhamu Mkuu wa Kituo cha Polisi Mwanga na Askari wa kituo kidogo cha polisi Nyumba ya Mungu na Lang'ata Wilayani kutokana na tuhuma za rushwa dhidi yao.
Mghwira ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,ametoa agizo hilo leo Julai 21,wakati akizungumza kwenye mkutano wa Hadhara katika Kata ya Lang'ata,Wilaya ya Mwanga.
Katika Mkutano huo ambao, uliohudhuriwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, na viongozi wengine wa chama na serikali,Mghwira amesema Askari hao wamekiuka taratibu na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa,hatua ambayo imekuwa kikwazo kikubwa katika jitihada za kudhibiti uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Amesema Askari hao wamejianzishia vituo vyao vya ushuru na kuanza kukusanya mapato yatokanayo na uvuvi haramu katika Bwawa la Nyumba ya Mungu,ambalo lilifungwa baada ya kukithiri kwa uvuvi haramu na samaki kupotea.
"Naomba niseme Askari wa Lang'ata na Nyumba ya Mungu mmenikwaza,kwani kituo chenu kipo juu na mtu hata awe mfupi kunizidi anaweza kuona mazingira yote ya Bwawa na kuona wavuvi haramu,lakini wao huwa hawawaoni, hii ni hatari sana,naomba RPC uwaondoe mara moja na kuwachukulia hatua,"amesema Mghwira.
Mkuu huyo ambaye alitangaza kulifungua Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa Muda,alisema serikali ilikuwa na nia njema kulifunga Bwawa hilo,lakini Askari wamepoteza malengo ya serikali na kukwamisha mpango wa kuacha samaki wawe wakubwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Polepole alisema serikali haitawavumilia askari au watendaji watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuchafua utendaji mzuri wa Serikali ya awamu ya Tano.