Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma, inamshikilia Luka Nkini (38) mkazi wa Airport jijini Dodoma kwa tuhuma za kujipatia Sh1.5 milioni na mali nyingine kwa njia ya udanganyifu.
Kamanda Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo akizungumza jijini hapa juzi alitaja mali nyingine alizopata mtuhumiwa huyo kinyume cha sheria ni viwanja viwili, mashamba mawili, vifaa vya kieletroniki na samani.
Kibwengo alisema Nkini alijipatia vitu hivyo kutoka kwa kina mama 10, baada ya kuwadanganya kuwa ana uwezo wa kuwaongezea maradufu fedha na vitu walivyompa.
“Mtuhumiwa alijifanya ni mjukuu wa babu mitimingi wa Kigoma na amekuwa akifanya uhalifu huo katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Kilimanjaro, huku akitoa sharti la kutaka kushiriki ngono na baadhi ya kina mama hao” Kibwengo
“Mtuhumiwa amekiri na kuwataja washiriki wenzake ambao ni Hussein Mvungi (44) mkazi wa Homo Kilimanjaro naye tunamshikilia. Mwingine ni John Munuo mkazi wa Sanya Juu Kilimanjaro ambaye tunamtaka kuripoti ofisi yoyote ya Takukuru iliyopo karibu naye kabla rungu halijamfikia,” Kibwengo.