RAIS Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale aliyeaga dunia Jumanne jijini Dodoma.
Rais Samia alieleza kusikitishwa na taarifa ya kifo cha Mfugale na kuwa daima atakumbuka mchango wake katika ujenzi wa miundombinu hasa barabara, madaraja, reli na umeme.
“Pole kwa familia na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mwenyezi Mungu amweke mahali pema peponi, Amina,” aliandika Rais Samia katika ukusara wake kwenye mtandao wa kijamii wa ‘twitter.’
Mwili Mfugale unawasili Dar es Salaam leo jioni kwa ndege kutoka Dodoma na utaagwa kesho katika Viwanja vya Karimjee.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Tanroads, Hija Malamla, alisema jana kuwa, leo jioni mwili utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo kuhifadhiwa.
Alilieleza gazeti hili kuwa, mwili huo utakuwa Karimjee kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 11 jioni ili kutoa nafasi kwa watu kuuaga.
Malamla alisema kesho jioni utapelekwa nyumbani kwake Kimara Temboni ambako utalala na keshokutwa asubuhi utapelekwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Rita wa Kashia kwa ajili ya misa na pia, familia na majirani kuuaga.
Alisema saa 10 jioni mwili utaondolewa kanisani kuanza safari ya kwenda kijijini kwake Ifunda Iringa kwa njia ya barabara.
Malamla alisema mwili huo ukifika Iringa taratibu nyingine za kifamilia zitaendelea na Jumatatu utapumzishwa katika nyumba ya milele katika makaburi ya familia.
Mhandisi Mfugale aliondoka Dar es Salaam Jumatatu jioni kwenda Dodoma kikazi na alipokuwa kwenye kikao katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, alianza kujisikia vibaya na kuomba kupelekwa hospitali na aliaga dunia wakat akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma.
Kati ya mambo ya kukumbukwa kwa Mfugale ni pamoja na kutengeneza mfumo wa usimamizi wa madaraja nchini aliposhiriki kikamilifu ujenzi wa madaraja mbalimbali likiwamo Daraja la Magarasi lenye mita 178 kwa Sh milioni 300.
Pia amejenga Daraja la Mkapa, Daraja la Umoja linalounganisha Tanzania na Msumbiji lililopo mkoani Ruvuma, Daraja la Rusumo lililopo mkoani Kagera, Daraja la Kikwete lililopo Magarasi na Daraja la Kigamboni- Dar es Salaam.
Mwaka 2014 alisajiliwa kuwa Mhandisi Mshauri na kuwa mwanachama wa Chama cha Wahandisi Tanzania.
Amesaidia ujenzi wa madaraja mengi nchini hatua iliyomfanya Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, kuamua kuliita daraja linalounganisha Barabara ya Mandela na Nyerere jina la Daraja la Mfugale.
Katika utendaji wake amebuni na kusimamia barabara za kitaifa zenye urefu wa takriban kilomita 36,258. Amekuwa Mwenyekiti wa kikosi cha ujenzi wa Reli ya kisasa SGR inayoendelea kujengwa,na alikuwa mjumbe wa timu ya majadiliano ya miradi mikubwa ya umeme.