Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mengi atimiza ahadi kwa mwanaye, azindua kitabu

10595 Mengi+pic TanzaniaWeb

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi amezindua kitabu kinachoelezea harakati na mafanikio yake katika maisha ikiwa ni matokeo ya ushauri wa mwanaye.

Kitabu hicho kilichozinduliwa jana kinachoitwa I Can, I Must, I will amekiandika Mengi mwenyewe na uzinduzi huo ulihudhuriwa na Rais John Magufuli.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mengi alisema alihamasishwa kuandika kitabu hicho na mwanaye, Rodney (sasa marehemu) ambaye alimtaka siku moja awe na kitabu kinachoelezea harakati na mafanikio yake.

Alisema alimuahidi mwanaye kufanya hivyo.

“Ninafurahi leo nimetimiza ahadi yangu kwa mwanangu. Ahadi nyingine ni ya kwenda ‘gym’ kila siku, kwa sasa ninakwenda mara tatu kwa wiki, nitaanza kwenda kila siku,” alisema Mengi.

Alisema alizaliwa kwenye familia maskini na ndiyo iliyomsukuma kujituma hadi kuwa mfanyabiashara mkubwa. Mengi alisema alijifunza mambo mengi kutoka kwa mama na kaka yake ambao walikuwa wafanyabiashara wadogo.

Mfanyabiashara huyo ambaye ni mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), pia aliwatangaza washindi wa shindano alilokuwa akiliendesha kwenye mitandao ya kijamii ambao ni Wakonta Kapunda wa Tanzania na Brian Mwenda kutoka Kenya.

Wakonta ni msichana aliyepooza kutokana na ajali aliyoipata akiwa mwanafunzi na aliandika wazo la biashara kwa kutumia ulimi kwa kuwa mikono yake haifanyi kazi yoyote.

Washindi hao walijishindia Dola 20,000 za Marekani (zaidi ya Sh45 milioni) kila mmoja kutoka kwenye shindano la Dream to Greatness aliloliendesha Mengi.

Rais Magufuli alimchangia Wakonta Sh10 milioni kwa ajili ya kumsaidia kutekeleza mawazo yake.

Akizungumzia ushindi wake, Wakonta alimshukuru Mengi kwa kutoa nafasi ya watu kushiriki kwenye shindano hilo, akisema atatumia fedha alizoshinda katika wazo lililompatia ushindi.

Hata hivyo, mshindi huyo hakutaka kuweka wazi wazo lililompatia ushindi kwa madai kwamba bado hajalifanyia kazi. Alisisitiza kwamba amekuwa akifanya kazi ya kuandika miswada (scripts) na fedha hizo atazitumia kwenye malengo hayo. “Siwezi nikasema wazo kwa sasa kwa sababu bado hatujalifanyia kazi, lakini nitazitumia kwa same purpose (lengo kusudiwa),” alisema Wakonta ambaye kwa sasa anaishi Mbeya.

Alichosema Rais

Katika uzinduzi wa kitabu hicho, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kutokatishwa tamaa katika kazi wanazozifanya, badala yake wafanye kazi kwa bidii na wawe wavumilivu katika changamoto wanazopitia katika kujiletea maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz