Mbunge wa Jimbo la Tiverton na Honiton nchini Uingereza Neil Parish yupo chini ya uchunguzi kutokana na kitendo chake cha kuangalia video za ngono akiwa Bungeni.
Mashuhuda wawili ambao ni wabunge wa kike wanadai walimuona Parish akiangalia video za ngono katika matukio mawili tofauti, kwanza alikuwa anaangalia akiwa Bungeni katika vikao vya kawaida lakini pia akaangalia tena kwa mara ya pili katika kikao cha kamati.
Katika hatua nyingine mke wa mbunge huyo amemtetea mume wake kwa kudai kuwa ni mtu mwema na hajawahi kuwa na tabia hiyo ingawa amesisitiza kuwa watu hawatakiwi kuangalia video za ngono kwani ni udharirishaji kwa wanawake.
Kutokana na kashfa hiyo mbunge Neil Parish amekubali kuwa atakuwa tayari kutoa ushirikiano wote kwa wahusika wa uchunguzi huku akikiri kuwa alifungua file hilo kwa bahati mbaya.
Kumekuwa na wito kutoka kwa waheshimiwa mbalimbali wakimtaka Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kumuwajibisha kwa kumuondoa madarakani.
Wabunge wengine hasa wa kike akiwemo Harriet Harman Kutoka chama cha Labour amemtaka ajiuzulu wadhifa wake kwani hafai kuwa mbunge na haoneshi picha nzuri kwa jamii.
Waziri Rachel Maclean amepigilia msumari kuwa mbunge huyo anatakiwa kujiuzulu mara moja akisema:
“Aina hizi za tabia hazina nafasi katika mazingira yoyote yale ya kazi ya Bunge lolote lile, Lakini kila mtu lazima atambue kuwa inapotokea shutuma ya jambo lolote lile siyo kazi yetu sisi kunyoosheana vidole bali ni mamlaka husika kuchukua hatua.”
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kwa mara ya kwanza ameliongelea tukio hilo kwa kudai kuwa ni jambo ambalo halikubaliki katika mazingira yoyote yale ya kazi kuanzia ngazi ya juu hadi ngazi ya chini ya utendaji kazi.