Wanahabari waliokamata nyumba ya Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamechuana naye mahakamani wakati wa usikilizwaji wa shauri la kupinga nyumba hiyo isiuzwe.
Vilevile, Mbowe alitaka alipwe gharama za shauri hilo kutokana na nyumba yake kuingwa kwenye kesi ambayo yeye si mhusika.
Shauri hilo limesikilizwa leo Jumanne, Machi 12, 2024 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mary Mrio, ambapo Mbowe amewakilishwa na wakili wake, John Mallya, huku wajibu maombi wakijiwakilisha wenyewe.
Ingawa wanahabari hao wamelazimika kuiachilia nyumba hiyo na kuyaondoa mahakamani maombi yao ya kuikamata, wamepinga hoja ya Mbowe ya kutaka alilipwe gharama za shauri hilo huku wakibainisha wanachodai kiliwafanya waikamate nyumba hiyo, wakiamini ni ya mdaiwa.
Badala ya nyumba hiyo, wamesema watachukua hatua nyingine dhidi ya mtoto wa Mbowe, Dudley Mbowe wanayemdai.
Nyumba hiyo ya ghorofa moja iliyoko katika kiwanja namba 9, Mtaa wa Feza, Mikocheni B ilikamatwa Februari 28, 2024 na dalali wa Mahakama, kampuni ya MM Auctioneer & Debt Collectors kwa amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Mahakama hiyo iliamuru kukamatwa na kupigwa mnada nyumba hiyo kufuatia maombi ya wadai kufuatia shauri la maombi ya utekelezaji wa tuzo ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iliyotolewa kwa waliokuwa wafanyakazi wa gazeti la Tanzania Daima, Paul Maregesi na wenzake tisa.
Waombaji walifungua shauri hilo dhidi ya mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe, baada ya kushindwa kutekeleza tuzo hiyo ya CMA, ya kuwalipa malimbikizo ya mishahara yao yanayofikia Sh62.7 milioni.
Baada ya mdaiwa kushindwa kufika mahakamani mara tatu, ndipo wanahabari hao waliiomba mahakama, nayo ikaamuru wakakamata nyumba hiyo waliyoiainisha kama mali ya mdaiwa, ili ipigwe mnada na fedha zitakazopatikana zilipe deni lao.
Kufuatia hatua hiyo iliyoainisha nyumba yake, Mbowe alifungua shauri la maombi mahakamani hapo, dhidi ya wanahabari hao, mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima (mwanaye Dudley) na dalali wa mahakama akipinga kukamatwa na kupigwa mnada kwa nyumba hiyo.
Shauri hilo liliposikilizwa leo, Wakili Mallya ameileza mahakama kuwa mteja wake Mbowe anapinga hatua ya kukamatwa kwa nyumba hiyo kwa kuwa ni mali yake na si ya mdaiwa (Dudley).
Pia Mallya amesema kuwa mteja wake (Mbowe) si sehemu ya shauri la maombi ya utekelezaji tuzo baina ya wanahabari hao dhidi ya mkurugenzi wa Tanzania Daima, Dudley.
Vilevile Mallya amesema kuwa Mbowe amewasilisha na hati ya nyumba hiyo, kuthibitisha uhalali wa umiliki wake na akahitimisha kuwa kwa hali hiyo, mteja wake anaomba pia alipwe gharama za shauri hilo.
Akijibu hoja hizo mmoja wa wajibu maombi, Kulwa Mzee, kwa niaba ya wenzake, ameieleza mahakama kuwa baada ya kupitia nyaraka za shauri la Mbowe na viambatanisho vyake, wamekubaliana na maombi ya Mbowe ya kuiachilia nyumba hiyo.
“Mheshimiwa, tumepitia nyaraka zote na viambatanisho, tumejiridhisha na tumekubaliana kwa pamoja kwamba hiyo ambayo tuliikamata ni ya familia, lakini inamilikiwa na Freeman Mbowe na kwamba mkurugenzi tunayemdai Dudley Mbowe si mmiliki,” amesema Kulwa na kuongeza.
“Kwa hiyo tunaiomba mahakama tuiondoe hiyo nyumba kwenye maombi yetu.”
Kuhusu kumlipa Mbowe gharama za shauri hilo, Kulwa amesema kwa uelewa wao kwa mashauri ya migogoro ya kikazi hauna gharama kutokana na uwezo wa vipato vidogo vya wafanyakazi.
Amesema kuwa wakati wanachukua hatua hiyo walikuwa wakiamini nyumba hiyo ni ya mdaiwa kwa sababu katika hatua ya makubaliano alikuwa anawambia wakutane na kufanya vikao nyumbani kwake na kwamba katika nyumba hiyo ndipo walipokuwa wakifanyia vikao hivyo.
Kulwa amesisitiza kuwa katika hatua za mwisho, mwombaji katika shauri hilo (Mbowe), aliwaalika wakutane hapohapo ambapo walikuwa wanakutana na wakurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima, pamoja na yeye, na kuwa alikubali kubeba dhamana ya deni la mwanaye kuwa angewalipa yeye deni Desemba 2023.
Hivyo, amesema kwa hali hiyo waliamini kuwa hapo ndipo nyumbani kwake mdaiwa wao, na kwamba baada ya kushindwa kuwalipa katika kutafuta namna ya kupata haki yao ndio maana waliamua kukamata hiyo nyumba.
“Kwa hiyo tunoamba tusilipe gharama (za kesi) na tunaomba kila mmoja abebe gharama zake”, amesema Kulwa.
“Kwanza huyu mwombaji (Mbowe) hajaingia gharama kwani katika hatua zote za majadiliano tulikuwa tunakwenda kwake kwa gharama zetu, na ahadi zake za kutulipa Desemba baada ya kushindwa kutekeleza hilo ilituathiri, maana tulikuwa katika maandalizi ya sikukuu na ada za watoto shuleni.”
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya udalali ya iliyokamata nyumba hiyo, ambaye ni mjibu maombi wa 11 katika shauri hilo, Jesca Massawe alijiondoa katika kuwajibika kwa maombi hayo ya Mbowe.
Jesca amesema yeye kama dalali wa mahakama na ofisa wa Mahakama alipokea amri ya Mahakama ikimwelekeza kukamata nyumba hiyo.
Amefafanua madalali wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yao walikaa na mahakama hiyo chini ya Jaji Mfawidhi, akawaelekeza kuwa katika mashauri hayo ya kukamata mali, wasijihusishe na utambuzi wa mali, bali wakamate na kama kuna changamoto basi ipelekwe mahakamani.
“Kwa hiyo sisi tulitekeleza amri ya Mahakama kama tulivyoelekezwa,” amesema Jesca.
Akijibu hoja hizo, Wakili Mallya amesema anakubaliana na wajibu maombi kuwa wameamua kuachia nyumba hiyo.
Hata hivyo, kuhusu suala la gharama, Malya amesisitiza kuwa mteja wake anastahili kulipwa gharama na kwamba mambo mengine aliyoyasema mjibu maombi alipaswa kuyaleta kwa njia ya kiapo.
Kuhusu hoja za mjibu maombi wa 11, Jesca, Mallya amesema ni kweli ni ofisa wa Mahakama lakini maelezo yake kwamba walielekezwa kuwa hawana wajibu wa kufanya utambuzi wa mali wanayokwenda kuikamata, ni maneno tu yaliyotolewa mahakamani badala ya kiapo.
Amesema kwa kuwa anamtaja na Jaji Mfawidhi, haya yalipaswa kuwasilishwa kwa njia ya kiapo na si maneno matupu mahakamani.
“Kwa hiyo naiomba Mahakama yako isiyazingatie na tunaomba izingatie suala la gharama,” amesisitiza Mallya.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Msajili Mrio ameahirisha shauri hilo mpaka kesho, Jumatano, Machi 13, 2024 saa 8 mchana kwa ajili ya uamuzi.
Shauri la msingi
Kuhusu shauri la msingi, lililofunguliwa na wanahabari hao la maombi ya utekelezaji wa tuzo ya CMA, Paul kwa niaba ya wenzake ameiomba mahakama hiyo kuyaondoa kwa ajili ya kuleta mengine upya na Mahakama imekubaliana nao na kuamuru yaondolewe kwa kibali cha kuyaleta tena.
Sakata lilivyoanza
Awali wanahabari hao walifungua shauri la mgogoro wa kikazi namba 28461 la mwaka 2023, CMA dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, baada mwajiri wao huyo kudaiwa kuvunja mikataba yao ya ajira, wakiomba kulipwa malimbizo ya mishahara yao jumla ya Sh114 milioni.
Hata hivyo CMA katika uamuzi wake uliotolewa na Mwenyekiti Bonasia Mollel Julai 17 mwaka 2023, iliamuru wadai walipwe Sh62.7 milioni baada ya pande mbili kukaa pamoja na kujadiliana na kufikia makubaliano, suala ambalo halikutekelezwa na hivyo wakafungua shauri la maombi ya utekelezaji wa tozo hiyo.