Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kufanya maandamano katika makao makuu ya mikoa nchi nzima, hadi pale Serikali itakapotekeleza madai Yao ya upatikanaji katiba Mpya, mifumo huru ya uchaguzi na kutatua changamoto ya ugumu wa maisha.
Akitangaza ratiba ya maandamano hayo, Leo tarehe 6 Machi 2024, mkoani Mtwara, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amesema yataanza tarehe 22 Hadi ,30 Aprili mwaka huu.
“”Baada ya maandamano makubwa na yaliyofanikiwa ya Majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha; sasa tunaingia katika hatua ya pili itakayohusisha wiki ya maandamano katika Makao Makuu ya Mikoa yote Nchi nzima yatakayoanza tarehe 22 hadi 30 Mwezi Aprili, 2024,” amesema Mbowe.
Mwenyekiti huyo wa Chadema amechanganua madai yao zaidi ya 10 ambayo yamewafanya kuendeleza maandamano hayo ikiwemo kuundwa kwa Tume Huru ya uchaguzi na kubadilishwa kwa mfumo mzima wa kuendesha na kusimamia chaguzi zote nchini.
Mengine ni, kubadilishwa kwa mfumo mzima wa kutenga Majimbo ya uchaguzi ili kuhakikisha kwamba Majimbo ya uchaguzi yanazingatia idadi sawa ya Watu wanaowakilishwa. Kubadilishwa kwa mfumo mzima wa uandikishaji wa wapiga kura ili kuhakikisha kwamba kila mwenye sifa ya kupiga kura anaandikishwa kama mpiga kura na kuondoa masharti ya kibaguzi ya kuandikisha Wapiga Kura.
“Mengine ni kubadilishwa kwa mfumo mzima wa uteuzi wa Wagombea ili kukomesha vitendo vya kuengua Wagombea wa Upinzani.Kubadilishwa kwa mfumo wa uendeshaji wa kampeni za uchaguzi ili kukomesha vitendo vya kunyanyasa Wagombea wa Vyama vya Upinzani na kuwezesha matumizi sawia ya Vyombo vya Habari,” amesema Mbowe.
Kubadilisha mfumo mzima wa gharama za uchaguzi na namna ya kuusimamia na mfumo mzima unaohusu maadili ya uchaguzi na namna ya kuyasimamia ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa Wagombea wa Upinzani kwa kisingizio cha maadili ya uchaguzi.
Mengine ni, kubadilisha utaratibu wa upatikanaji na uapishaji wa mawakala wa Vyama au Wagombea na utaratibu wa kupiga na kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi. Kuweka mfumo mpya na bora zaidi wa kutatua migogoro yote ya uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa Uchaguzi.
Mbowe ametaja madai mengine kuwa ni Kubadilisha utaratibu wa uteuzi wa Madiwani na Wabunge wa Viti Maalum na Kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowezesha Wagombea Binafsi kushiriki katika uchaguzi kama Wagombea katika ngazi zote za uchaguzi.