Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbowe akimbilia mahakamani kunusuru nyumba ‘yake’ waliyoikamata wanahabari

Nyumba Ya Mbowe.png Mbowe akimbilia mahakamani kunusuru nyumba ‘yake’ waliyoikamata wanahabari

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekimbilia mahakamani kunusuru kupigwa mnada nyumba anayodai kuwa ni mali yake iliyokamatwa kwa amri ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, akiweka pingamizi dhidi ya amri hiyo.

Nyumba hiyo ya ghorofa moja iliyoko katika kiwanja namba 9, Mtaa wa Feza, Mikocheni B, jijini Dar es Salaam ilikamatwa Februari 28, 2024 na dalali wa Mahakama, kampuni ya udalali ya MM Auctioneer & Debt Collectors, kwa amri ya Mahakama.

Mahakama hiyo iliamuru kukamatwa na kupigwa mnada nyumba hiyo kutokana na maombi ya wadai katika shauri la maombi ya utekelezaji wa tuzo ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iliyotolewa kwa waliokuwa waandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Paul Maregesi na wenzake tisa.

Maregesi na wenzake walifungua shauri hilo mahakamani hapo dhidi ya mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe, baada ya kushindwa kutekeleza tuzo hiyo ya CMA, kuwalipa deni la malimbikizo ya mishahara yao Sh62.7 milioni.

Baada ya mdaiwa huyo Dudley kushindwa kufika mahakamani mara tatu, ndipo wanahabari hao waliiomba Mahakama, ikaamuru wakakamate nyumba hiyo waliyoiainisha kama mali ya mdaiwa wao, mtoto huyo wa Mbowe, (Dudley), ili ipigwe mnada.

Hata hivyo, Mbowe naye amefungua shauri la maombi mahakamani hapo dhidi ya wanahabari hao, mkurugenzi huyo wa gazeti la Tanzania Daima (mwanaye Dudley) na dalali huyo wa Mahakama akipinga kukamatwa na kupigwa mnada kwa nyumba hiyo.

Shauri hilo la maombi la Mbowe limetajwa mahakamani hapo mbele ya Naibu Msajili Mary Mrio, leo Alhamis, Machi 7, 2024 na Mbowe amewakilishwa na wakili wake, John Mallya huku wajibu maombi (wanahabari hao) wakijiwakilisha wenyewe.

Wakili Mallya ameieleza Mahakama hiyo kuwa msingi wa shauri hilo ni kuomba kuachiliwa kwa nyumba hiyo kwa kuwa si mali ya mdaiwa katika shauri hilo la maombi ya utekelezaji (mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima – Dudley), bali ni mali ya mteja wake Mbowe.

Amesema katika hati ya maombi iliyoambatana na kiapo, pia wameambatanisha na hatimiliki ya nyumba hiyo inayoonesha nyumba hiyo inamilikiwa na mteja wake, Mbowe.

Kwa niaba ya wajibu maombi, Maregesi ameieleza Mahakama kweli wamepata nyaraka za shauri hilo na kwamba walizipata jana, hivyo akaomba wapewe muda wa kuzipitia, huku akiungwa mkono na mwenzake, Kulwa Mzee ambaye ameomba muda wa siku 15.

“Katika nyaraka walizotuletea kuna kiapo na vielelezo vingi, kwa hiyo tunaomba muda wa kutosha kuzipitia ili nasi tulete counter affidavit (kiapo kinzani) na tunaomba kuleta majibu yetu ndani ya siku 15,” amesema Mzee.

Hata hivyo, baada ya majadiliano na maelekezo ya mahakama pande zote zimekubaliana na Mahakama imeamuru wajibu maombi hao kuwasilisha mahakamani hapo majibu yao dhidi ya maombi hayo ya Mbowe, kabla ya Machi 12 na imepanga kusikiliza shauri hilo Machi 12, 2024.

Dudley Mbowe

Katika hati kiapo chake, Mbowe kinachounga mkono maombi yake hayo anadai alisajiliwa kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo Februari 4, 2010 na kwamba tangu wakati huo amekuwa akiitumia nyumba hiyo kwa makazi.

Anadai alipata taarifa za kukamatwa kwa nyumba hiyo Februari 15, 2024 kupitia mitandao ya kijamii, hivyo akamuandikia barua Wakili Mallya kwenda kudurusu mahakamani jalada hilo la maombi ya utekelezaji wa tuzo ya CMA, kujua hasa nini kilichotokea mahakamani.

Mbowe anadai hana uhusiano wowote wa kikazi na wajibu maombi (wanahabari hao) na kwamba yeye hajashtakiwa nao katika mahakama yoyote ya kisheria nchini kwa madai yoyote ya jinai au ya madai.

Vilevile anadai yeye si sehemu ya wadaawa katika shauri hilo la maombi ya utekelezaji baina ya wanahabari hao na mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima.

Hivyo anaiomba mahakama hiyo ifanye uchunguzi kubaini usahihi wa ukamataji wa nyumba hiyo kwa ajili ya utekezaji wa shauri la maombi ya utekezaji (tuzo ya CMA) na ichunguze kama yeye alikuwa ni mdaawa katika shauri hilo.

Kisha anaiomba Mahakama hiyo baada ya uchunguzi huo itamke kuwa kukamatwa kwa nyumba hiyo si halali na ni batili na iwaamuru wajibu maombi walipe gharama halisi alizozitumia mpaka tarehe ya kuachiliwa kwa nyumba hiyo na nafuu nyingine kadri Mahakama itakavyoona inafaa.

Katika shauri la maombi ya utekelezaji lililofunguliwa na wanahabari hao, wakati lilipoitwa leo, mjibu maombi yaani mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima/ Dudley hakuwepo mahakamani yeye mwenyewe wala mwakilishi wake.

Hivyo, Mahakama hiyo imeahirisha na kupanga kuendelea nalo katika hatua ya usikilizwaji Machi 12, 2024.

Mwanzo wa sakata hilo

Awali, wanahabari hao walifungua shauri hilo la mgogoro wa kikazi namba 28461 la mwaka 2023, CMA Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, baada mwajiri wao huyo kuvunja mikataba yao ya ajira, wakiomba kulipwa malimbizo ya mishahara yao jumla ya Sh114 milioni.

Hata hivyo, CMA katika uamuzi wake uliotolewa na Mwenyekiti, Bonasia Mollel Julai 17 mwaka 2023, iliamuru wadai walipwe Sh62.7 milioni baada ya pande zote kukaa pamoja na kujadiliana na kufikia makubaliano ya pamoja.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu kila mwisho wa mwezi wa Oktoba, Desemba 30, 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa Februari, 2024, lakini hakutekeleza ahadi hiyo ndipo wakafungua shauri la maombi ya utekelezaji.

Dudley hajawahi kufika mahakamani mara zote ambazo shauri hilo lilipangwa kusikilizwa yaani Februari 9, 13 na 14, 2024 ndipo wanahabari hao wakaomba Mahakama iamuru nyumba hiyo waliyitaja kama yake ikamatwe na Mahakama ikatoa amri hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live