Mweyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Aikael Mbowe amezungumza na waandishi wa habari leo Augosti 22, 2024 Jijini Dar es Salaam na kusema kuwa masuala ya utekaji, mauaji yamekithiri zaidi nchini.
Mbowe amesema kuwa wao kama chama wameamua kupaza sauti kuwataka wenye maamlaka nchini kutambua thamani ya maisha ya kila Mtanzania.
“Leo nitazungumza mambo mawili mahususi ambayo sisi kama Chama tunaamini yanagusa Watanzania na yanazua taharuki na hofu, nitazungumza kuhusu sakata la wimbi kubwa la Viongozi wa CHADEMA, Watanzania wengine wasio na Vyama wanaoendelea kutekwa na Vyombo vya Usalama vya Nchi yetu na Vyombo hivyo vikaendelea kukaa kimya, kuwateka Watu katika taratibu ambazo sio za kisheria, kutowafikisha Vyombo vya Kimahakama kwa utaratibu wa kisheria na wengine kuuawa”
“Tumeamua tupaze sauti kuwataka wenye Mamlaka Nchini kutambua kwamba thamani ya maisha ya kila Mtanzania mwenzetu ni kubwa kuliko chochote, kwahiyo sisi kama Jamii ya Tanzania ni wajibu wetu kusimama kuhakikisha haki kwa Watu wote inapatikana na tusiendelee kuruhusu baadhi Vyombo vya Dola viendelee kuwaua , kuwatesa na kuwapoteza Watanzania na sisi tukakaa kimya, lazima tuseme na tunasema kwa kujiamini na tunasema tukijiua kwamba athari zake ni nini hata kwa maisha yetu binafsi lakini lazima tuseme ili hatimaye ukatili huu usionekane kama ni mzaha au ngonjera”
“Siku za hivi karibuni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilitoka na tamko kuhusu kuongezeka kwa utekaji nyara, TLS walitoka na orodha kubwa ya Watu zaidi ya 80 kwa majina na maeneo waliyotoka, taarifa ya TLS imetoka August 09 mwaka huu ikionesha majina ya Watu waliotekwa na walipotekewa na wengine waliokutwa wamekufa katika vyumba vya kuhifadhi maiti, inapotoka taarifa hii halafu Vyombo vya Dola vikakaa kimya ili ni jambo ambalo limetulazimisha sisi kuungana na TLS kupasa sauti” — Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe leo Jijini Dar es salaam akiongea na Waandishi wa Habari.