Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazito ‘mwalimu wa figo’

26358 MWALIMU TanzaniaWeb

Sat, 10 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Mgonjwa wa kwanza kupandikizwa figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prisca Mwingira ameelezea maisha yake akitaja hisia za chanzo cha tatizo lake, huku akiwasilisha ombi maalumu serikalini.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu mjini Morogoro jana, Prisca (31)aliyezungumza kwa mara ya kwanza tangu alipotoka Muhimbili Desemba 2,2017 baada ya kupandikizwa figo Novemba 21, alisema licha ya kufurahi kurudi katika hali nzuri ya kiafya anapata shida kufuatilia matibabu.

Alisema kukaa mbali na hospitali ni tatizo kubwa kwake, lakini pia mumewe kuwa mbali na kituo anachofanyia kazi.

“Namshkuru Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amenisaidia mpaka nimefika hapa, lakini naomba nipeleke ombi langu kwa Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako anisaidie labda kutoka hapa kufundisha mpaka kuhamia kwenye ofisi zingine ambazo zipo kwenye kada ya ualimu,” alisema Prisca ambaye ni mwalimu katika Sekondari ya Nanenane.

Mmoja wa walimu katika shule hiyo, Rose Chabariko alisema Prisca anakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo vumbi la chaki na wakati mwingine hujisikia vibaya, hivyo jukumu lao kubwa ni kumsaidia.

Mkuu wa shule, Sarah Madabi alisema alimpokea mwalimu huyo akitokea Sekondari ya Mikese iliyopo Morogoro Vijijini Agosti 23, lakini “anahitaji msaada mkubwa aweze kuwa vizuri kwa sababu nimekaa naye kipindi kifupi, lakini nimebaini changamoto nyingi zinamkabili. Nimempatia ruhusa amehudhuria kliniki si chini ya mara tatu Muhimbili.”

Alisema, “Mapendekezo yangu kama wizara (ya Elimu), Serikali imwangalie kwa kumpunguzia kazi hii ya kufundisha, kama kuna sehemu yoyote anaweza kupata ya kujishikiza ambayo ni rafiki kwake wampeleke huko, sisi kwa mazingira yetu ya sasa yanampa shida, anatumia chaki ambazo kwake ni tatizo.”

Historia ya tatizo

Akizungumza historia ya tatizo lake, Prisca alisema Agosti, 2016 akiwa kazini huko Mikese alianza kuvimba mwili.

“Nilianza kuvimba mwili na hata nilipokuwa nikikaa miguu ilikuwa inavimba na baadaye kuishiwa pumzi, nilivyokwenda hospitali kupima wakaniambia nina tatizo la figo na lilishafikia hatua ya mwisho,” alisema.

Prisca alichangiwa figo na mdogo wake, Batholomeo Mwingira (28). Hata hivyo, baada ya mafunzo kutoka kwa madaktari kwa muda mrefu, anaamini chanzo cha figo zake kufeli ni matumizi holela na ya muda mrefu ya dawa za kupunguza maumivu mwilini.

Chanzo: mwananchi.co.tz