Mariam, mtoto wa aliyekuwa mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ali Kibao akizungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni (kulia), baada ya kufika kuwafariji kwa kifo cha baba yake.
Kibao aliuawa baada ya kutekwa na watu wenye silaha, jioni ya Ijumaa ya Septemba 6, 2024 eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa ndani ya basi la Kampuni ya Tashriff kwenda mkoani Tanga.
Baada ya kuondoka naye akiwa amefungwa pingu, mwili wake uliokotwa eneo la Ununio, Dar es Salaam ukiwa na majeraha na inaelezwa alimwagiwa tindikali usoni.
Leo Jumanne, Septemba 10, 2024, Waziri Masauni amewasilisha salamu za rambirambi za Serikali na kutoa Sh5 milioni huku akieleza familia jinsi Rais Samia alivyoguswa na tukio hilo na tayari wamekwisha kuanza uchunguzi ili kuwabaini wahusika.
Mariam kwenye maelezo yake amesema: “Tumesikia Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya uchunguzi vifanye uchunguzi wa kifo cha baba yetu, sisi kama familia tutakuwa tunapataje taarifa za uchunguzi huo, najua kuna muda inakuwa ni vigumu kuwafikia viongozi wa juu huko serikalini hasa kwa kesi kama hii ni jambo nzito.”
Tunachoomba ni ushirikiano wenu kama Serikali kwetu sisi maana hata sisi hatujui nani amefanya huo utekaji na mauaji ya baba yetu. Muhimu tunaomba huo uchunguzi ufanyike kwa haraka ili ukweli ujulikane na haki ipate kutendeka,” ameongeza Mariam.
Waziri Masauni amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia na ameiomba familia hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wamempoteza mpendwa wao huku akiwaomba wawe na subira ili vyombo husika vikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kutekwa na kuuawa kwa mzazi wao.