Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda awataka Mbowe, Lissu na Mnyika "Nitakuja peke yangu"

Msafara Wa Makonda Wasimamishwa Ilemela Makonda awataka Mbowe, Lissu na Mnyika "Nitakuja peke yangu"

Sun, 14 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuzindua vuguvugu la kudai haki Tanzania 2024 na kueleza kwamba hawaamini tena CCM katika maridhiano, CCM imemjibu ikisema anapotosha umma yeye akiwa ni mnufaika mkubwa wa maridhiano yaliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Jana, Mbowe alisema alimwamini Rais Samia kwenye maridhiano, kwamba tangu wameanza mazungumzo, Rais huyo amekuwa haziishi R nne alizoziasisi, hivyo hawaamini tena CCM lakini chama hicho cha upinzani kitaendelea kuamini katika maridhiano.

Akizungumza maridhiano baina ya CCM na Chadema, Mbowe alisema yalikuwa yamefika hatua nzuri na hata CCM walikiri kuwa uchaguzi uliopita, wa Serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu 2020 haukuwa huru na haki.

Rais Samia kwa mara ya kwanza, alikutana na Mbowe Machi 4, 2022, Ikulu ya Dar es Salaam saa chache baada ya Mbowe kuachiwa huru kutoka gerezani alikokaa kwa miezi minane kwa tuhuma za ugaidi.

Kikao chao kilifungua milango ya vikao vingine baina ya viongozi wa vyama hivyo vilivyoendelea kwa nyakati tofauti kuyasaka maridhiano ya kisiasa.

Mei 2022, kamati ya watu 10 kutoka Chadema iliundwa na idadi kama hiyo kutoka CCM na zilikutana Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kuanza mazungumzo hayo, Hatua iliyochukuliwa kama ukurasa mpya kwa siasa za Tanzania.

Mwaka mmoja baadaye, vyama hivyo vilianza kuonyesha hali ya kutoaminiana na viongozi wake walijitokeza hadharani kunyoosheana vidole.

Makonda amjibu Mbowe

Akijibu yaliyozungumzwa na Mbowe leo Januari 14, 2024, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda amesema Taifa limeshuhudia Rais Samia akipambana kujenga umoja na mshikamano wa Taifa, hivyo wanamshangaa Mbowe kumtweza.

“Kwa masikitiko makubwa jana tumepata nafasi ya kumsikia kaka yetu Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema akituhumu na kutoa kauli za kudhalilisha na kufedhehesha na kutweza utu wa kiongozi wetu bila kujali dhamira njema aliyoonyesha mwenyekiti wetu wa CCM, Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa umoja na mshikamano katika Taifa letu.

“Taifa hili kwa mara ya kwanza limeshuhudia haki ikisimamiwa kikamilifu ikiwa pamoja na jitihada binafsi za mwenyekiti wetu wa CCM na Rais wa Tanzania alizozifanya katika kuunda Tume ya Haki Jinai kupitia mambo kadhaa wa kadhaa ili kuhakikisha kwamba Mtanzania anapata haki yake bila kujali rika, elimu kipato, kabila, dini na hata kule alipotokea,” amesema Makonda.

Makonda amesema hoja ya Mbowe kwamba mapendekezo yaliyotolewa na kikosi kazi, mapendekezo yaliyotolewa na CCT pamoja na yaliyotolewa na baadhi ya vyama vya siasa yote yamepuuzwa, si kweli.

“Mbowe anafahamu katika mapendekezo 84 yaliyotolewa, 63 yote yamechukuliwa na yapo kwenye muswada ambao hatua za kisheria zinaendelea katika kuunda kwa sheria na yeye ni mnufaika mkubwa wa maridhiano ambayo yamemfanya akawa yupo huru dhidi ya kesi zote za kisiasa na kuachiwa huru bila masharti.

“Ya yeye mwenyewe na chama chake na vingine wanafanya mikutano ya hadhara bila kubugudhiwa tena kwa mlinzi mkali chini ya Jeshi la Polisi, ili kuhakikisha dhamira ya Rais Samia inatimia si tu kwa vyama vya siasa bali kwa Watanzania wote,” amesema.

Makonda ameomba kwamba kabla Chadema hawajaandamana akutane na Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika na makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu wafanye mdahalo utakaoandaliwa na wanahabari ili kila upande ueleze yao.

“Nitapenda uje na timu yako, mimi nitakuja peke yangu ili ueleeze yale ambayo unayakusudia kuwapeleka Watanzania barabarani na mimi niyaseme yetu ili sasa Watanzania wachague kwenda barabarani kuvuruga uchumi wa Taifa lao au kubaki kujenga maridhiano na umoja wa kitaifa,” amesema.

Hizo blaa blaa

Alipotafutwa kuzungumzia kauli za CCM, Mbowe amekiita kilichosemwa na Makonda kuwa “blaa blaa kwa kuwa hakijajielekeza kwenye hoja zilizozungumzwa.”

Amefafanua kwamba katika mkutano wake na waandishi wa habari hakuzungumza masuala ya kutonufaika na maridhiano, bali yake alijikita kwenye mambo matatu yanayoifanya Chadema iandamane.

“Mimi nilijikita kwenye mambo matatu ambayo ndiyo yanayotufanya tuandamane. Moja ni mabadiliko ya kisiasa yanayohusisha hii miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni.

“Mbili ni hali ya umasikini na ugumu wa maisha kwa Watanzania na tumeitaka Serikali ieleze mkakati wa kukabili hali hiyo, lakini jambo la tatu, tumeitaka Serikali ijifunze kusikiliza maoni ya wananchi,” amesema.

Amesema chama hicho na wadau wengine walitoa maoni kuhusu mabadiliko ya sheria hizo lakini Serikali haikusikiliza ndiyo maana imewasilisha bungeni miswada yenye kasoro zinazolalamikiwa.

Alipoulizwa kuhusu maridhiano baina ya vyama hivyo, mtaalamu wa masuala ya sheria, Fulgance Massawe amesema ni vugumu kumjua mnufaika kwenye mazungumzo yaliyokuwa yakifanywa baina ya vyama hivyo.

Akkifafanua, Massawe ameesema mikutano na maridhiano ya pande mbili hizo ilikuwa sirini, hivyo wanaojua aliyenufaika ni wawili wenyewe.

“Si rahisi leo hii kujua nani amenufaika, maridhiano lilikuwa jambo la siri wenyewe ndiyo wanaojua nani kanufaika nayo,” amesema Massawe ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Majeshi kufanya usafi siku ya maandamano

Kauli ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ya Jeshi la Wananchi na Jeshi la Polisi kufanya usafi Januari 23 na 24, tarehe iliyotangazwa na Chadema kuwa siku ya maandamano kitaifa, imeibua mjadala huku Chadema ikisisituiza maandamano yataendelea kama kawaida.

Akizungumzia hilo, Mbowe amesema usafi wa Jiji la Dar es Salaam hautazuia chama hicho kuendelea na shughuli zake huku akisisitiza kwamba maandamano yapo palepale.

Akizungumzia hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Conrad Masabo amehoji inawezekanaje vyombo vya ulinzi na usalama vifanye usafi ilhali kuna halmashauri zenye wajibu huo.

Hoja nyingine, aliyoibua ni iwapo mkuu wa mkoa ana mamlaka ya kikatiba ya kuviamuru vyombo vya ulinzi na usalama kufanya shughuli ya usafi.

“Ukitoka huko unajiuliza ni lazima tufanye utafiti tujue kama kulikuwa na mpango awali wa ratiba hiyo ya usafi au la,” amehoji.

Hata hivyo, alieleza kikatiba shughuli za usafi haziwezi kuzuia shughuli zozote na kwamba si polisi wote watakwenda kwenye kazi hiyo.

“Kama kuna polisi watabaki na maandamano yataratibiwa vizuri, maana yake yatafanyika na watakuwepo kuyalinda,” amesema.

Lakini, alieleza nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia ilipaswa kujipanga kumlinda anayeandamana kuhakikisha anafikisha ujumbe wake.

“Kama nchi inaheshimu maoni ya wananchi na utawala wa sheria ilikuwa vizuri kupishanisha shughuli hizo,” alisema.

Maoni ya wadau mtandaoni kuhusu maandamano Januari 24

Chanzo: www.tanzaniaweb.live