Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana na kuzungumza na Balozi wa Switzerland nchini Mhe. Didier Chassot leo tarehe 7 Mei 2024 katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Katika Mazungumzo yao viongozi hao wamejadili namna kukuza na kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya ulinzi na usalama kwa maslahi ya pande zote mbili na Jumuiya ya Kimataifa.
Pia wamejadili jinsi ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu athari za migogoro inayojitokeza sehemu mbalimbali duniani na kutoa mapendekezo yenye tija kwa jumuiya ya kimataifa juu ya namna bora ya kutatua migogoro hiyo ili kupunguza adhari zake kwa jamii.
Aidha wamejadili programu mbalimbali zitakazochagiza kuimarika kwa ushirikiano huo ikiwemo ziara za mara kwa mara za viongozi wa sekta ya ulinzi na usalama na kuanda na kushiriki katika mikutano inayolenga kutatua migogoro.
Akizungumza katika mkutano huo Waziri Makamba ameeleza kuwa majadiliano ya utatuzi wa migogoro ni muhimu yakaangazia Bara la Afrika ambapo kwa muda mrefu Nchi nyingi kama vile DRC zimekuwa katika migogo na hazipewi kipaumbele katika mijadala ya kuleta amani inayojitokeza katika majukwaa mbalimbali ya Kimataifa.
Naye Balozi Chassot amesema Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika utatuzi wa migogoro na kuchangia jitihada za kuleta amani sehemu mbalimbali duniani na Switzerland inaitazama Tanzania kama mdau muhimu wa kushirikiana naye kati eneo hilo.
Balozi Chassot ametoa pole kwa Watanzania kwa hasara na uharibufu uliojitokeza kutokana na athari za mvua kubwa zilizosababisha mafuriko katika sehemu mbalimbali nchini na kusababisha vifo,majeruhi, uharibu wa makazi na mali za watu na miundombinu.