Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amekanusha taarifa zilizotolewa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusu kuanzishwa kwa noti ya pamoja ya Afrika Mashariki.
Makamba kupitia taarifa aliyoitoa katika ukurasa wake wa X (zamani Twitter), amesema taarifa hizo si za kweli na mapendekezo yaliyopo hatua hiyo itafikiwa mwaka 2031.
"Hizi taarifa si za kweli. Taratibu na vigezo vya kiuchumi na kitaasisi vya kufikiwa kwa Umoja wa Fedha (Monetary Union)/Sarafu Moja (Single Currency) kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki bado kukamilika. Mapendekezo ni kufika hatua hiyo mwaka 2031," ameandika Makamba.
Uvumi huo umeenea katika mtandao wa X kupitia ukurasa uliorasmiishwa kwa matumizi ya kiofisi (grey tick) unaoitwa #Government of East Africa.
Mwananchi inaomba radhi kwa kuripoti taarifa hiyo ambayo chanzo cha awali hakikuwa rasmi.