Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesema Tanzania haitachoka kupeleka askari wake kulinda amani katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kwa sababu inaamini katika uhusiano wa kindugu, uliowekwa na waasisi wa taasisi hiyo.
Akizungumza na mabalozi wa nchi za Sadc wanaowakilisha nchi zao jijini Beijing, China jana, Makamba alisema msingi huo wa kifalsafa ndiyo uliofanya Tanzania sasa iwe na askari katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Msumbiji baada ya kuombwa kufanya hivyo na nchi wenyeji.
“Nimekuja hapa kuzungumza nanyi na kuwahakikishia kwamba msimamo wa Tanzania kuhusu Sadc haujawahi kuyumba na hautabadilika. Tatizo lolote litakaloikumba nchi ya Sadc litachukuliwa kuwa pia ni tatizo la Tanzania wakati wote,” alisema.
Suala la Tanzania na nafasi yake katika kulinda amani liliibuliwa na mwakilishi wa Balozi wa DRC nchini China, Francois Balamuene, aliyeishukuru Tanzania kwa kupeleka vikosi vyake nchini mwao na kusema imeonyesha urafiki na ujirani wa kweli miongoni mwao.
Makamba ambaye yuko katika ziara ya kikazi nchini China kufuatia mwaliko aliopewa na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, alisema Sadc ni jumuiya imara kulinganisha na nyingine kwa sababu msingi wake ulijengwa katika falsafa na misingi imara.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wa nchi 14 za Sadc waliohudhuria mkutano huo, Balozi wa Namibia nchini China, Elia Kaiyamo, alisema wamefurahi kusikia maneno ya Makamba kwa vile yameakisi maneno yaliyowahi kutamkwa zamani na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusu umuhimu wa nchi za Sadc kuwa pamoja.
“Leo tumeona kwamba wewe ni mwanafunzi wa Mwalimu Nyerere kwa sababu ulichozungumza ndiyo yalikuwa maneno yake kila wakati alipopata nafasi ya kuzungumza na wanachama wengine wa Sadc. Tuendelee kuwa wamoja na umoja wetu ndiyo utasaidia kupambana na changamoto zetu,” alisema.
Sadc ni jumuiya ya ushirikiano wa nchi 16 zilizoko Mashariki na Kusini mwa Afrika ambayo kuanzishwa kwake kulihusishwa na harakati za kudai uhuru.
Nchi wanachama wa Sadc ni Angola, Botswana, Comoros, DRC, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Ushelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia and Zimbabwe.
Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa baadhi ya nchi wanachama wa Sadc kama vile, Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji na Zimbabwe. Ni moja ya nchi waasisi wa jumuiya hiyo.
Tanzania ilikuwa kitovu cha harakati za ukombozi wa mataifa ya kusini hasa baada ya kuanzishwa kwa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika iliyoongozwa na Brigedia Jenerali Hashim Mbita kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 1994.
Hata baada ya kamati hiyo kuvunjwa, Tanzania imeendelea kusaidia mataifa mengine hasa katika masuala ya ulinzi kwa kutoa askari wake kwenda kupambana na vikosi vya Serikali, kwenye mataifa hayo dhidi ya vikundi vya wapiganaji vinavyoathiri amani kwenye nchi hizo.
Baadhi ya nchi za Sadc ambazo vikosi vya Tanzania vimekwenda kuimarisha ulinzi ni pamoja na Msumbiji na DRC ambako hadi sasa kuna vikosi vya askari wa Tanzania wanaoimarisha ulinzi na usalama.