WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Maji Maji na Tamasha la Utalii wa Utamaduni, linalotarajiwa kufanyika mjini Songea Mkoa wa Ruvuma kuanzia Februari 25 hadi 27,mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa tamasha hilo limeandaliwa na taasisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Baraza la Mila na Desturi la Mkoa wa Ruvuma na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Litazinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro Februari 25, mwaka huu.
Kilele cha Tamasha hilo kitakuwa Februari 27, mwaka huu na Waziri Mkuu atakuwa mgeni rasmi na wageni mbalimbali kutoka Malawi na Zambia wanatarajiwa kuhudhuria.
Dk Lwoga alisema malengo ya maadhimisho hayo, ambayo hufanyika kila mwaka Februari 27 ni kuwakumbuka mashujaa waliopigana Vita vya Maj iMaji na kufa wakitetea maslahi mapana ya nchi. Mashujaa 67 walinyongwa na wakoloni mjini Songea Februari 27, 1906 na kuzikwa katika makaburi yaliyopo Makumbusho ya Maji Maji.
“Tamasha linalenga kutoa fursa kwa wananchi wa Tanzania kuenzi, kutunza, na kuendeleza urithi wa utamaduni na wa asili kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo,” alisema Dk Lwoga
Tamasha hilo linalenga kuthamini mchango wa wazee na viongozi waliotangulia, akiwemo marehemu Dk Lawrence Gama katika kuleta maendeleo ya mkoa wa Ruvuma na ukanda wa Nyanda za Juu Kusini katika kuinua uchumi na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.
Alisema ili kuenzi wazee, kauli mbiu ya maadhimisho mwaka huu ni “Maisha ya Wazee Wetu, Fahari Yetu.”
Dk Lwoga alisema maadhimisho hayo, yataambatana na programu mbalimbali za kielimu mashuleni na maeneo ya wazi, maonesho ya wajasiriamali na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu historia ya nchi yetu na kuhamasisha jamii kutumia na kurithisha urithi wetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alisema alisema kuwa kutakuwa pia na kampeni ya michango ya hiari kutoka kwa wadau mbalimbali kwa lengo la kuboresha miundombinu ya uhifadhi na huduma za Makumbusho ya Maji Maji.
Dk Lwoga alitoa wito kwa wananchi kuhudhuria maadhimisho na tamasha hilo muhimu kwa historia ya nchi yetu.