Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua jengo jipya la hospitali ya Aga Khan Machi 9, 2019 ikiwa ni baada ya kukamilika kwa upanuzi wa hospitali hiyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi 5, 2019 mwakilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) nchini Tanzania, Amir Kurji amesema mradi wa upanuzi wa huduma za afya za Aga Khan umegharimu Dola 83 milioni.
Amesema sehemu ya hospitali iliyopanuliwa itajishughulisha na mafunzo na rufaa na itakuwa na vitanda 170 kutoka vitanda 75 vilivyokuwepo awali.
"Programu za kisasa za matibabu ya maradhi ya moyo, saratani, sayansi ya neva, afya ya mama na mtoto, zote hizo zikisaidiwa na uchunguzi unaotumia teknolojia ya kisasa vitaiwezesha Tanzania kupata huduma za afya zenye hadhi ya kimataifa hapa hapa nyumbani," amesema Kurji.
Mwakilishi huyo amesema inatarajiwa kwamba hospitali hiyo itasababisha uwepo wa utalii wa kitabibu kwa kuwezesha watu wa nchi za jirani kuja Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu yao.
Amesema hospitali ya Aga Khan imepata uthibitisho kutoka Shirika la Joint Commission International linalothibitisha viwango vya juu vya kimataifa katika ubora wa huduma zilizo salama.
Kurji pia amesema kwamba wamepata idhini ya kujenga vituo vya afya Dodoma na Mwanza.
Amesema upembuzi yakinifu na michakato mingine kuhusiana na miradi hiyo inaendelea na wanatarajia hospitali hizo zitaanza kazi mwishoni mwa mwaka 2020.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Hussein Kidanto amesema hospitali hiyo itatumiwa na wanafunzi wa chuo hicho kupata mafunzo kwa vitendo yatakayoimarisha weledi wao.
"Tuna wanafunzi 28 wanaosomea fani ya udaktari chuoni kwetu, kati yao watatu wanatoka nje ya nchi, wengine wote ni Watanzania.”
“Wanafunzi hawalipi hela yoyote, wanasoma kwa msaada wa Aga Khan ili kuwajengea uwezo wakahudumie jamii," amesema Profesa Kidanto.
Mkurugenzi Mkuu wa Tiba na Afya wa Taasisi ya utoaji huduma za afya Tanzania kutoka AKDN, Dk Ahmed Jusabani amesema upanuzi huo umeboresha mfumo wa afya wa Aga Khan na si katika majengo pekee.
Amesema hospitali hiyo ndiyo hospitali binafsi iliyo bora hapa nchini na itafanya kazi kama hospitali ya rufaa.
Amesema gharama za matibabu ni za kawaida ikilinganishwa na gharama za matibabu yanayotolewa nje ya nchi.