Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa kushiriki swala ya Eid Dar

4590ea42f63e75bd02f60dbc0b2ba93a.jpeg Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa atashiriki swala ya Sikukuu ya Eid-El-Adh’aa kitaifa, itakayofanyika Julai 21 katika Msikiti wa Mtoro, jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma, ilimnukuu Mutfi na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi ikieleza kuwa, swala hiyo itaswaliwa saa 1.30 asubuhi na baadaye kufuatiwa na Baraza la Eid itakayofanyika hapo hapo mara baada ya swala hiyo.

“Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania anawatakia Waislamu na wananchi wote sikukuu njema na ameomba kusheherekea kwa salama na amani, huku tukiendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na virusi vya corona,” ilieleza taarifa hiyo.

Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum jana aliwataka Waislamu watakaojaaliwa wafanye ibada ya kuchinja mnyama ili kutekeleza matakwa ya sikukuu hiyo inayowakumbusha kumbukumbu ya kisa cha Nabii Ibrahim alipoagizwa na Mungu kumchinja mwanawe Ismail.

Alisema ibada hiyo ya kuchinja wanyama kama ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, inaweza kutekelezwa kwa siku tatu kuanzia siku ya sikukuu.

“Tunawaomba waumini wote kujitokeza kwa wingi katika kutekeleza ibada hiyo kubwa ya sikukuu ya Eid huku tukitakiana amani, upendo na utulivu na zaidi kumuomba Mwenyezi Mungu ili aweze kutuepusha na janga la corona katika taifa letu,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz