WAKUU wa mikoa nchini leo wanatarajiwa kuwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kumueleza ni kwa nini bei ya saruji ilipanda.
Julai 16 mwaka huu baada ya Rais John Magufuli kumuapisha kwenye viwanja vya Ikulu, Chamwino Dodoma, Majaliwa alitoa siku nne kwa viongozi hao wawasilishe taarifa kwake na akawaonya wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya saruji waelewe kwamba serikali haijalala.
“Na ilimradi wakuu wa mikoa wako hapa, niwape mpaka tarehe 20 kila mmoja aende palipo na kiwanda, palipo na mawakala wa saruji waangalie ni kwa nini bei ya saruji imepanda kutoka bei ya kawaida hadi ongezeko la zaidi ya shilingi elfu tatu mpaka elfu nne bila sababu yoyote ile wakati Serikali haijaongeza kodi, miundombinu tumepeleka, makaa ya mawe yapo ya kutosha, labour ile ile,”alisema Majaliwa.
Alisema ongezeko la bei halikubaliki na hakuna sababu za msingi kwa kuwa serikali kwa miaka mitano iliyopita imefanya mambo makubwa kujenga miundombinu ili wafanyabiashara wafanye kazi kwa urahisi.
Wiki kadhaa zilizopita aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki walifanya kikao na wazalishaji wa saruji kujadili fursa, changamoto na namna bora ya kukuza sekta ya ujenzi kupitia saruji.
Katika kikao hicho kwenye ofisi za Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), jijini Dar es Salaam Bashungwa aliwasihi wasipandishe bei ya saruji kiholela hasa kuzingatia kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya 5 ni kuiona Tanzania inakua nchi ya viwanda.
Katika kikao hicho, mawaziri hao walikutana na kampuni tisa za saruji ikiwemo Dangote Cement, Camel Cement, Nyati Cement, Mbeya Cement, Kilimanjaro Cement, Maweni Cement, Tanga Cement, Lake Cement, Twiga Cement na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).
Mawakala na wauzaji wa saruji mkoani Kigoma jana walimweleza Mkuu wa Mkoa huo, Thobias Andengenye kuwa hawafichi saruji ili kupandisha bei ya bidhaa hiyo na kwamba, kiasi wanachopata kutoka kiwandani ni kidogo kuliko mahitaji.
Wakala wa saruji kutoka viwanda vya Tanga na Simba Cement vya Tanga, Kilahumba Kivumo alisema amekuwa akipata taabu kupata saruji kutoka kiwandani kulingana na mahitaji yake na jana hakuwa na hata mfuko wa saruji wakati kuna wateja ambao tayari wameshalipia kwake.
Mkurugenzi wa ghala la kuhifadhi saruji la Rubibi Enterprises lililopo Gungu mjini Kigoma, Asha Juma alimuelza Andengenye kuwa wana tatizo la upatikanaji saruji kutoka kiwandani.
Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na uuzaji wa saruji rejareja, Raymond Ndabhiyegese alisema anapata shida kukidhi mahitaji ya wateja wadogo kwa kuwa anapata saruji kidogo kuliko kiwango anachoagiza kutoka kwa wakala.
Andengenye alisema watafuatilia kuona kama kauli za wafanyabiashara hao zina ukweli na kwamba wamekuta maghala mengi ya kuhifadhi na kuuza saruji ni matupu hakuna saruji.
Alisema katika ziara hiyo pia wabaini kuwepo tatizo la usafirishaji wa saruji kwa sababu ya kutopatikana mabehewa lakini pia kuchelewa kwa mzigo njiani.
Andengenye alisema watazifanyia kazi taarifa hizo na amewaonya wafanyabiashara watakaouza saruji kwa bei ya juu kuwa watachukuliwa hatua kali.