Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa awataka vijana kujikita kilimo cha bustani

B416d64216c462ba9d40093b45b3b155 Majaliwa awataka vijana kujikita kilimo cha bustani

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kuacha kukaa vijiweni na badala yake waanzishe Kilimo cha bustani ili kujiongezea kipato.

Alitoa wito huo jana wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namahema alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu unaolenga kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo.

“Biashara ya bustani inalipa sana, yeyote anayetaka fedha, ataipata shambani. Nataka niwasisitize sana twende tukalime, twende shambani. Shamba siyo lazima ulime mahindi, mpunga pekee ama muhogo. Bustani ya nyanya, vitunguu, karoti na mchicha inalipa sana,” alisema.

Amesema Serikali imetoa Sh milioni 600 ili zijenge masoko na kuongeza uzalishaji kwenye mabonde ya Mpumbe (kata ya Nkowe), Mnindu (Nandagala), Chiepo (Mnacho) na Chikalala (Chibula).

“Serikali imewaandalia mradi huu ili mlime bustani wakati wote, iwe masika au kiangazi. Rais wetu ametoa fedha hizi ili vijana na akinamama walime bustani na kujipatia kipato zaidi,” amesema.

Pamoja na ushauri huo Waziri Mkuu Majaliwa pia aliagiza kamati ya ujenzi ya mradi huo irekebishe mara moja kasoro zilizosababishwa na ukiukaji wa taratibu wa ujenzi wa majengo ya serikali.

Alimtaka msimamizi wa mradi huo, Kalistus Mnunduma ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nkowe ahakikishe anatoboa milango ya ziada kwenye jengo ili kuongeza usalama wa watumiaji wakati wa kutoka na kuingia kwenye soko hilo.

Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kubaini ujenzi wa soko hilo ulianza kwa kutumia michoro ya awali (sketch) badala ya kutumia ramani za ujenzi na matokeo yake wakajenga jengo lenye vyumba vya baridi vya kuhifadhia mazao, eneo la wazi la kupokelea mazao na kuweka mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea.

“Nimetoa maagizo manne. Kwanza, toboa milango, pili weka vizimba ili wananchi wauze bidhaa zao mahali pasafi, usiruhusu watu wauze bidhaa zao chini, siyo sawa kiafya.

Tatu, chimba visima, weka mnara, tangi na mipira ya kumwagilia ya kutosha ili wakulima wasipate taabu ya kusomba maji. Weka mashine ya kusukumia maji ili uweze kuyasambaza katika eneo kubwa.

Nne, tenga eneo la kuuza bidhaa kwa rejereja ili wananchi wa hapa jirani wanufaike na mradi huu,” alisema.

Pia alimuagiza Ofisa Kilimo wa Wilaya hiyo, Harun Ibrahim Kiara ahakikishe anatoa elimu ya kilimo cha bustani kwa vijana ili waanze na matuta machache. “Pia anzisheni programu ya kukutana na vijana na wanawake mwaeleze bonde la Mnindu linatumikaje kwa kilimo hicho,” alisema.

Mapema, akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Selemani Mrope alisema: “Mradi huu umelenga kuwezesha kuwepo kwa soko la uhakika, ongezeko la ajira na uzalishaji, ongezeko la kipato kwa jamii, upatikanaji wa uhakika wa chakula lishe na uboreshiji wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya bustani,” alisema.

Aidha alisema Chuo cha Ufundi Stadi Mkowe kinatekeleza mradi huyo kwa kuingiza kipengele cha kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo wa mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu kwa ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kupitia mfuko wa kuongeza na kuboresha elimu (SDF).

Mrope alisema hadi sasa wamekamilisha kazi ya kuandaa mitala na miongozo ya kufundishia wakulima wote wa bustani kwa gharama ya Sh 4,000,000 na kwamba wanaendelea na ukarabati wa darasa moja litakalotumika kutoa elimu kwa wakulima wote wa bustani ambalo gharama yake ni Sh milioni 4.2.

Chanzo: habarileo.co.tz