Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka mawaziri na viongozi wengine wa Serikali kutumia vizuri mitandao ya kijamii ili kuepuka mambo ambayo jamii haikubaliani nayo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 3, 2018 wakati akifungua mafunzo ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa jijini Dodoma.
“Jana nimewaambia mawaziri wote tuliojiunga katika mitandao hii tuitumie vizuri, wewe kama kiongozi wa Serikali unatakiwa kusoma kilichoandikwa kwenye mtandao na kuona umuhimu wa kwenda kuchangia ama la,” amesema Majaliwa.
Kwa upande wake ofisa mtendaji mkuu wa taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema programu hiyo ya mafunzo ya uongozi, ni ya kwanza na ya aina yake iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili ya viongozi hao.
“Lengo la programu hii ni kuimarisha uwezo wa wakuu wa mikoa na makatibu tawala katika kufanya uamuzi wa kimkakati, kuongoza watu na kusimamia rasilimali nyingine, pamoja na kujijengea sifa binafsi za uongozi,” amesema.