Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa awataka Watanzania kutambua umuhimu wa kura zao

2d21e5b5ac7265b66643299f8c538f5b Majaliwa awataka Watanzania kutambua umuhimu wa kura zao

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watambue umuhimu wa kura zao watakapokuwa wanachagua viongozi Oktoba 28, mwaka huu.

Majaliwa aliyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kilindoni katika Wilaya ya Mafia mkoani Pwani kwenye mkutano wa kampeni. “Tambua umuhimu wa kura yako.

Uongozi wa nchi hautaki majaribio, unaweza kufanya majaribio kwa viongozi wa vikao vya harusi au send-off lakini siyo uongozi wa nchi,” alisema Majaliwa

Katika mkutano huo, Majaliwa alimwombea kura mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Mafia, Omari Kipanga na mgombea udiwani Kata ya Kilindoni, Salum Ally.

“Lazima tumpe urais mtu ambaye tunamjua kwa historia, ambaye amewahi kuongoza kikundi cha watu na akapata mafanikio. Tunataka tumchague Rais ambaye anayeweza kutuletea maendeleo na si maneno tu.

Tumebakiza siku 21 tu, tunataka kiongozi ambaye kwa dhamira yake mwenyewe anamtanguliza Mungu mbele,” alisema na kuongeza: “Nawaletea viongozi kutoka chama ambacho ni taasisi madhubuti yenye kuweka mipango yake kwenye Ilani yake ya uchaguzi.

Watakuja wagombea mbalimbali hapa, wasikilizeni, wapimeni lakini tambueni umuhimu wa kura zenu”. Alisema Watanzania wanapaswa kumchagua Rais atakayetambua kuwa rasilimali za nchi ni mali za Watanzania na si za hao anaowafahamu yeye.

“Viongozi wa CCM ninaowaleta kwenu wana mambo ya kueleza. Wanaeleza ni nini wamefanya katika miaka mitano iliyopita na nini watafanya katika miaka mitano ijayo.

“Tunatafuta kiongozi wa nchi ambaye ametulia, anayekwenda kuongoza watu zaidi ya milioni 60 wenye dini tofauti, makabila na itikadi tofauti, tunatafuta kiongozi ambaye anaweza kuzitunza tunu za Taifa ikiwemo amani,” alisema Majaliwa.

Akielezea kuhusu uboreshaji wa barabara, Majaliwa amesema Sh bilioni mbili zimetolewa kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, ya muda maalumu na madaraja kadhaa katika Halmashauri ya Mafia.

“Matengenezo ya kawaida yamefanyika katika barabara za Kilimahewa – Mdundani (km 2), Jimbo – Jojo (km 10), Baleni – Kipingwi (km 6.4) na matengenezo ya maeneo korofi yamefanyika katika barabara za Ndogoni - Kimtondo; Baleni - Kipingwi, na Mwambae – Tumbuja. Pia matengenezo ya muda maalum yamefanywa katika barabara za Marimbani – Utende (km 4.2) na Baleni – Kilombero (km 8.3),” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz