WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaonya raia wapya wa Tanzania wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini kuacha kujihusisha na uhalifu ikiwamo kuingiza silaha kinyume cha sheria.
Raia hao wapya ni ambao awali walikuwa wakimbizi kutoka Burundi na kuomba uraia wa Tanzania wakiendelea kuishi katika makazi ya wakimbizi ya Mishamo, Wilaya ya Tanganyika na Mishomo Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi.
Majaliwa alitoa onyo hilo juzi alipokuwa akihutubia raia hao wanaoishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Mishamo wilayani Tanganyika.
"Zipo taarifa baadhi ya wakimbizi kutoka Burundi wanaoishi kwenye makazi hayo na wale waliopewa uraia wa Tanzania wanajihusisha na visa vya kihalifu ikiwamo kuingiza silaha za kivita nchini kimagendo na kufanya ujangili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi na Mahale,” alisema.
Aliagiza kuundwa kamati za ulinzi na usalama katika kila kijiji kilichopo kwenye makazi hayo ya Mishamo ili zisaidie kuwaripoti watu ambao wanaingia nchini kinyemela na kujificha kwenye makambi hayo.
"Mwaka jana ilifanyika operesheni kwenye makazi ya Mishono ya kuwasaka wahalifu, silaha zaidi ya 100 huku 30 zikiwa za kivita zilikamatwa.”
"Pia kiligunduliwa kiwanda kimoja cha kutengeneza silaha za kienyeji kwenye makazi hayo. Naonya visa hivi visijirudie," alisema Waziri Mkuu.
Aliwataka wanaoishi katika kambi hiyo wafanye kazi za halali kwa bidii na kuonya ambao wameomba uraia wakisubiri kuhakikiwa wakibainika kujihusisha na uhalifu hawatapewa uraia wa Tanzania.
"Serikali haipendi kuona makazi ya wakimbizi yanakuwa sehemu ya uvunjifu wa amani, hivyo ni vyema muende pamoja na serikali katika kusimamia amani na mfuate taratibu za watu kuingia nchini na kutoka kwani serikali haikatazi mtu kuingia wala kutoka bali kinachotakiwa ni kufuata taratibu," alisema.
Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda, aliwaonya wakimbizi hao kuwa endapo watakuwa na tabia hiyo itakuwa vigumu kupatiwa uraia wa Tanzania wa kudumu.
Aliwataka wakimbizi wanaotaka kurudi kwenye nchi zao wafuate taratibu kwani milango ipo wazi kwa kuwa Burundi ina amani na uhusiano mzuri na Tanzania.
Majaliwa leo anahitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Katavi iliyoanza Agosti 25, mwaka huu.