Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa awaomba Singida wamchague JPM

0a8ebbaad5bc471ab8be7ab52c3f10a7 Majaliwa awaomba Singida wamchague JPM

Wed, 16 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba wakazi wa Singida wamchague Mgombea Urais wa CCM, Rais John Magufuli ili aongoze tena kwa miaka mitano na amalizie kazi zilizopangwa na CCM kwenye Ilani ya Uchaguzi.

Pia, amewataka wakazi wa Singida, watafakari wanataka kiongozi wa aina gani aiongoze Tanzania. Alitoa wito huo jana wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa kuwaombea kura wagombea wa CCM, akiwemo mgombea urais, Rais Magufuli.

“Uongozi wa nchi siyo jambo la mchezo, siyo jambo la kujaribiwa wala haliendi kwa upepo na ushabiki. Ni lazima mkae na kutafakari ni nani anafaa kuongoza nchi hii,” alisema Majaliwa katika Viwanja vya CCM Kata ya Ilongero wilayani Singida.

“Tukae tuangalie tulipo na tunapotaka kwenda. Tujiulize je, ni nani anaweza kutupeleka huko?”alisema. Aliwataka wakazi hao wajihadhari na wagombea wanaotumia majukwaa kutukana wenzao.

“Huu siyo wakati wa kutukanana bali ni wakati wa kuelezea sera na mambo gani atawafanyia” alisema Majaliwa na kuwaomba wakazi hao wa Singida wamchague Rais Magufuli “Nawaomba wanaIlongero, wana-Singida Kaskazini na wana-Singida wote ikifika tarehe 28 Oktoba mchagueni Dk Magufuli.

Sababu za kumuombea kura ni nyingi hasa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya kwa nchi hii. Wote mmeona na kusikia yaliyofanyika kwenye maeneo yenu,” alisema Majaliwa.

“Yeye ni mzuri wa kutabiri na kuyapangilia na kuyafuatilia. Yeye ni mzuri wa kutambua kero za wananchi wake na kuzitatua. Amejipambanua sana na kuwasihi wasaidizi wake wazingatie kuwatumikia Watanzania.

Sote tumeona, maendeleo yaliyopatikana ndani ya miaka mitano hayajapata kutokea,” aliongeza.

Pia alitumia fursa hiyo kuwaombea kura, Mbunge mteule wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo na mgombea udiwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru. Wakati huo huo, Majaliwa amempokea aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Singida, Frank Akunay ambaye ameamua kuhamia CCM.

Akunay amehamia CCM akiwa na mkewe, Betina Ibrahim na mdogo wake, Daniel Akunay. Akizungumza katika mkutano huo, Akunay alisema ameamua kurudi nyumbani kwa sababu zamani alikuwa CCM, lakini alipotea njia.

“Nimeamua kurudi nyumbani na nitachanja mbuga kuhakikisha CCM inashinda sababu mimi ni mtu wa field. Hapa Singida Kaskazini tuna vijiji 84, vitongoji 435 na kata 21.

Ninavijua vyote. Nakuhakikishia tutashinda kwa asilimia 98 sababu sijarudi kwa bahati mbaya,” alisisitiza Akunay. “Tuna uhakika wa kupata ubunge kwani anayegombea hatusumbui kabisa. Kwa madiwani, tumebakiza kata 19 kwani wawili walishapita bila kupingwa,” aliongeza.

Chanzo: habarileo.co.tz