Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa atoa ushauri Watanzania wanaosoma China

Video Archive
Fri, 31 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali ya Tanzania imewasihi wazazi wenye watoto wanaosoma nchini China kutowarejesha nchini humo hadi pale watakapopata taarifa za kidiplomasia kuhusu ugonjwa wa virusi Corona.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu watu 4,537 wameugua ugonjwa huo na zaidi ya watu 106 wamefariki dunia tangu ugonjwa huo uanze katika mji wa Wuhan uliopo jimbo la Hubei China Desemba 2019 hadi 28 Januari 2020.

Akijibu maswali ya papo kwa hapo leo Alhamisi Januari 30, 2020 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa zuio hilo wakati akijibu swali la papo hapo la Mbunge wa Mafinga Mjini (CCM), Cosato Chumi.

Chumi amehoji imejipangaje kudhibiti kuingia ugonjwa huo unaotokana na virusi vya Corona ambayo yasipothibitiwa unaweza kuathiri maendeleo ya nchi.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema Tanzania haina tatizo la Corona lakini jukumu ni kuweka tahadhari ambapo wameimarisha mawasiliano kati ya Tanzania na ubalozi nchini China.

Amesema Balozi wa China ametafuta madaktari ambao wamekuwa wakielimisha Watanzania walioko nchini humo kuhusu ugonjwa huo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Na balozi amewakanya Watanzania wasiwe na mizunguko mingi sana kwa sababu ugonjwa huo maambukizi yake ni pale watu wanapokutana,” amesema.

Amesema pia wametaarifu Watanzania wanapotaka kusafiri, watumie mawasiliano ya kimtandao ili kupata ridhaa ya vibali na kuambiwa hali ikoje badala ya kusafiri hadi mjini Beijing.

Amesema wanatambua kuna wazazi wana watoto wanaosoma nchini China na wengine wamesharejea likizo nchini.

“Tunawasihi watoto hao wasirejee nchini China hadi hapo tutakapopata mawasiliano ya kidiplomasia. Wizara ya Mambo ya Nje nchini Tanzania inaendelea kufanya mawasiliano na balozi mbili. Balozi ya Tanzania nchini China na balozi ya China nchini Tanzania,” amesema

Pale ambapo Serikali itaridhika kuwa hali imepungua basi itatoa tamko kwa watanzania waliopo nchini kurudi nchini China kuendelea na masomo vinginevyo watatafuta utaratibu mwingine

Majaliwa amewataka Watanzania kuwa makini na kila mgeni anayeingia nchini hasa wale walioko mpakani kutumia vifaa hivyo kubaini wale wenye dalili ya ugonjwa huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz