Chato. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza wakurugenzi wote nchini kutii haraka agizo lake la kuwaondoa maofisa kilimo waliopo kwenye ofisi za halmashauri na kuwapeleka vijijini kuwasaidia wakulima.
Waziri mkuu alitoa agizo hilo leo alipokua akizungumza na wananchi na viongozi wa mkoa wa Geita katika kata ya Nyamilembe wilayani Chato.
Alisema wapo wakurugenzi ambao hawajatii maagizo yake na kuwataka wakuu wa wilaya kusimamia hilo.
Majaliwa alisema halmashauri inapaswa kubaki na maofisa kilimo wawili tu ambao ni mkuu wa idara na wa bustani.
Aidha, aliwataka wakurugenzi kununua pikipiki kwa ajili ya maofisa kilimo vijijini ili waweze kuwatembelea wakulima na kuwashauri namna bora ya kulima, kutunza na kuwatafutia masoko ya uhakika.