Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika(Sadc), akishauri mapendekezo ya mkutano yaweke misingi ya kuondoa changamoto za utekelezaji wa malengo yatokanayo na mkataba wa uanzishwaji wake 1992.
Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi mwanachama zilishasaini itifaki mbalimbali katika kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya viwanda na mtangamano wa soko, maendeleo ya miundombinu kuwezesha mtangamano, ushirikiano katika ulinzi, usalama, demokrasia na utawala bora.
“Hatua zinachukuliwa lakini kasi inahitajika ili kufikia malengo yanafikiwa, changamoto tunazopitia ni nyingi ikiwamo tofauti za kisera, ufinyu wa bajeti na kimkakati baina ya nchi wanachama, gharama za kufanya biashara na ushiriki hafifu wa sekta binafsi,” amesema Majaliwa
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 18, 2020 wakati akifungua mkutano huo katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam uliotanguliwa na mkutano wa siku mbili wa Kamati ya Maofisa Wandamizi wa Sadc, uliowasilisha mapendekezo ya ajenda sita.
“Rais ambaye ni mwenyekiti wa Sadc alisema ‘malengo yaliyoasisiwa na wazee wetu katika uanzishaji wa jumuiya hiyo bado hayajafikiwa, iwapo juhudi za pamoja hazitachukuliwa basi itakuwa muda mrefu kufikia maendeleo, juhudi zinahitajika,” amesema Majaliwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema nchi hizo zimeendelea kukabiliwa na changamoto za migogoro ya kisiasa, mabadiliko ya tabia Nchi na majanga ya asili, ukuaji wa idadi ya watu, miji, hali ya huduma za elimu, afya, kasi ya ukuaji wa uchumi.
Pia Soma
- Zanzibar yatangaza kuzifunga shule, vyuo na madrasa
- MSD yazungumzia kupanda bei bidhaa za kujikinga na corona
- Dk Stergomena: Nchi tatu zinasuasua kuridhia soko la pamoja Sadc
Mtangamano huo unaongozwa na Mpango Mkakati Elekezi wa Kanda(RISDP) wa 2015/20 na awamu ya pili ya Mpango Mkakati wa Asasi za siasa, ulinzi na usalama inayofikia ukomo wake mwaka huu.
Mkutano huo unaoendeshwa kwa njia ya video umepokea ajenda sita kutoka Kamati ya Maofisa waandamizi wa mtangamano huo, ambazo ni taarifa ya maandalizi ya Dira ya Sadc 2050 na utekelezaji wa maazimio yaliyopita na Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Sadc 2020/2030.
Pia baraza hilo limepokea mapendekezo yatokanayo na hali ya michango na kifedha kwa ujumla ndani ya jumuiya hiyo, maadhimisho ya miaka 40 ya Sadc tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980.
Kabla ya kukutana kwa baraza hilo leo Machi 18, 2020 Jijini Dar es Salaam, mkutano mbalimbali ya mawaziri wa kisekta imefanyika ikiwamo mawaziri wanaohusiana na sekta ya uchukuzi na mawasiliano, utalii, Afya, kazi na ajifa pamoja na menejimenti ya maafa.