Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa atoa matumaini kwa watumishi wote wa umma

29532 Pic+majaliwa TanzaniaWeb

Fri, 30 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha masilahi ya watumishi wote wa umma wakiwamo wa kada ya afya kupitia Bodi ya Mishahara na Motisha baada ya kukamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi.

Amesema kukamilika kwa uhakiki huo wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma kutaiwezesha Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli kupanga upya mishahara na motisha kwa watumishi.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo jana jioni Alhamisi, Novemba 29, 2018 alipozungumza na watumishi wa Kituo cha Afya cha Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa uboreshaji miundombinu wa kituo hicho uliogharimu Sh500 milioni.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Waziri Mkuu, ilimnukuu Majaliwa  akisema Serikali inaendelea kushughulikia masilahi ya watumishi na kuwataka waendelee kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

“Tunataka mwananchi akifika kwenye maeneo ya kutolea huduma apokewe, asikilizwe na ahudumiwe,” amesema Majaliwa.

Majaliwa alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kujenga zahanati katika kila kijiji kwa kuwa wilaya hiyo imebakisha vijiji viwili kati ya 52 kumalizia ujenzi huo.

Waziri Mkuu amesema kwa sasa wananchi wa Ushirombo hawana sababu ya kusafiri umbali mrefu hadi Geita mjini au wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwa ajili ya kufuata huduma za afya kwa kuwa huduma zote zitakuwa zikipatikana kituoni hapo.

Amezitaja huduma ambazo zitakuwa zikipatikana kwenye Kituo cha Afya cha Ushirombo ni pamoja na za mama na mtoto, huduma za upasuaji wa aina zote mdogo na mkubwa, maabara, chumba cha kuhifadhia maiti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Dionis Myinga amesema ukarabati wa Kituo cha Afya cha Ushirombo ulianza Juni 22, 2018 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba, 2018.

Amesema lengo la mradi huo ni kukiwezesha Kituo cha Afya cha Ushirombo kutoa huduma bora za upasuaji wa dharura kwa kinamama wajawazito pindi wapatapo matatizo yatokanayo na uzazi. Majengo yote ya kipaumbele yamekamilika kwa asilimia 99.

Mkurugenzi huyo amesema mradi wa ukarabati wa kituo hicho cha afya unakadiriwa kutumia Sh436.933 milioni hadi utakapokamilika na Sh63.066 milioni zilizosalia kwenye ukarabati huo zitatumika kujenga njia za kuunganisha wodi na kukarabati majengo ya zamani.



Chanzo: mwananchi.co.tz