Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema nyumba zote zinazojengwa na taasisi za umma katika wilaya Kigamboni jijini Dar es Salaam zinapaswa kukamilika haraka ili ziuzwe ua kupangishwa kama ilivyokusudiwa.
Ameyasema hayo leo Jumatano, Novemba 27, 2019 baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF), Shirika la Nyumba za Taifa (NHC) na Watumishi Housing iliyopo katika wilaya ya Kigamboni.
Majaliwa amesema inasikitisha kuona kwamba watumishi wa umma na wananchi jijini Dar es Salaam hawana nyumba nzuri za kuishi wakati zipo nyumba nyingi nzuri zimejengwa na zinahitaji umaliziaji mdogo tu ili ziweze kukalika.
Hivyo, Waziri Mkuu ameitaka menejimenti ya NSSF kakamilisha haraka ujenzi na uwekaji wa miundombinu ya umeme, maji safi na maji taka katika nyumba zake 161 zilizoko Tuangoma, 820 zilizoko Mtoni Kijichi na 439 zilizoko Dungu ili ziuzwe na kuepusha uwezekano wa uharibifu unaoweza kutokea kwa nyumba hizo kakaa muda mrefu bila kupata wanunuzi au wapangaji.
Ili kufanikisha jambo hilo, Majaliwa amemtaka Mthamini Mkuu wa Serikali atathimini nyumba hizo na kutoa bei halisi ya soko kwa sasa ili kuwawezesha Watanzania wengi na hasa watumishi wa umma kununua na kupanga katika nyumba hizo.
Pia, Majaliwa amemtaka Mkuu wa wilaya na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni kuwasaidia watumishi wa wilaya na halmashauri hiyo kuingia mikataba rafiki itakayowawezesha watumishi hao kupewa kipaumbele katika kununua au kupanga kwenye nyumba hizo.
Majaliwa pia ameitaka menejimenti ya NSSF kufikiria namna ya kuzungumza na viongozi wa vyuo mabalimbali kama vile Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Mwalimu Nyerere ili wanafunzi wa vyuo hivyo wapatiwe fursa ya kupanga katika nyumba hizo kwa bei watakazomudu.
Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam ukishirikiana na Sumatra kuanzisha njia za mabasi ya daladala zitakazoanzia au kupitia kwenye nyumba za NSSF Mtoni Kijichi na Dungu ili kuwezesha wapangaji na wananchi watakaonunua nyumba hizo kupata usafiri wa umma.
Vilevile, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi huo kuhakikisha eneo la Mtoni Kijichi zilipojengwa nyumba za NSSF na NHC linapata huduma za Shule, Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi kwani litakuwa na wakazi wengi .
Ili kuongeza thamani ya nyumba hizo na kuvutia wapangaji na wanunuzi, Majaliwa ameitaka Menejimenti ya NSSF kuboresha barabara kwenye mitaa yote zilipojengwa nyumba hizo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura).
“Nashauri ziwekwe taa za sola kwenye barabara za mitaa yote ya nyumba hizi ili kupendezesha eneo na kuwafanya wananchi wahamasike kununua na kuishi katika nyumba hizi,” amesema Majaliwa.
Akiwa kwenye Mradi wa Nyumba za NHC Mtoni Kijichi, Majaliwa alitembelea Shule ya Awali ya Kids Paradise na kufurahishwa na utaratibu mzuri wa shirika hilo wa kukumbuka kujenga jengo zuri la shule hiyo na kulipangisha ili kuhakikisha kwamba watoto wanaoishi katika nyumba hizo wanapata fursa ya kusoma elimu ya awali.
Akizungumza baada ya kukagua Mradi wa ujenzi wa nyumba za NHC Mwongozo, Majaliwa ameutaka uongozi wa NHC kuwa karibu na wateja wanaopanga au kununua nyumba zao. “Shughulikieni malalamiko yote yanayotolewa na wateja wenu ili wajenge imani kwenu.”
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama alisema wizara yake imeyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kwamba watafanya kila njia ili kuhakikisha majengo yote yanakamilika haraka na kuuzwa au kupangishwa.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alimwambia Waziri Mkuu amekwishatoa maagizo kwa NHC ijenge uzio japo wa waya na wapande michongoma ili kuweka ulizi kwenye eneo la nyumba zao za Dungu.
Lukuvi alisema amewapa NHC miezi mitatu ili wafanye marekebisho katika nyumba ambazo zimelalamikiwa na wateja kuwa zina kasoro ili kujenga imani kwa wateja wao.
Mapemba Mkadiriaji Majengo wa NSSF, Abon Mhando ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Miradi wa NSSF alimwambia Waziri Mkuu kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba wa Tuangoma una jumla ya nyumba 161 na kati ya hizo nyumba 76 zimekamilika. Aliwataja wakandarasi wanaojenga mradi huo kuwa ni Kampuni za CASCO, Advent na NANDRA.
Alisema mradi wa Dungu una jumla ya nyumba 439 na kati ya hizo nyumba 95 zimekamilika na jumla ya makampuni 13 yameshiriki katika ujenzi wa mrdi huo.
Kuhusu mradi wa Mtooni Kijichi Mhando alisema mradi huo una jumla ya nyumba 820 na kati ya hizo nyumba 417 zimekamilika.