Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ataka viongozi kutatua kero za wananchi

77d34d6e22a3b55d37a4372e1895bf17 Majaliwa ataka viongozi kutatua kero za wananchi

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wote wa serikali, wahakikishe wanawafikia wananchi kwenye maeneo yao, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Alitoa kauli hiyo wakati akihitimisha Hoja ya kuliomba Bunge lijadili Hotuba ya Rais John Magufuli, aliyotoa wakati uzinduzi wa Bunge la 12, Novemba 13 mwaka jana.

“Tunapaswa kuwajibika kwa wananchi badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu wa kitaifa. Natumia fursa hii kuwaambia viongozi na watendaji wote wa serikali kuwa tutapima utendaji wenu kwa namna mnavyotatua kero za wananchi kwenye maeneo yenu,” alisema.

Majaliwa alitoa wito kwa kila mtendaji serikalini, ahakikishe anatimiza wajibu wake kikamilifu na serikali kwa upande wake itahakikisha inachukua hatua kwa wote watakaokiuka sheria, kanuni na taratibu za kazi na kamwe haitamvumilia mtumishi mzembe na mwenye kufanya kazi kwa mazoea.

Pia aliwataka viongozi mbalimbali kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali, ambayo wananchi wanatakiwa kujua utekelezaji wake.

Katika hilo, alinukuuu hotuba ya Rais Magufuli aliyotoa Juni 4, 2018 wakati akizindua Mpango wa Pili wa Kilimo wa Pili (ASDP II) kuwa watendaji wanatakiwa kutoa taarifa za utendaji wa miradi ili wananchi wajue utekelezaji wake.

Majaliwa alisema ipo miradi mingi ya kujivunia, ambayo serikali inatekeleza katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo ni lazima viongozi kutoa taarifa kuhusu utekelezaji huo kwa wananchi ili wajue nini kinaendelea.

Aliwaomba watendaji hasa wa serikali za mitaa, kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za serikali kuu katika kutekeleza miradi ya kipaumbele ambayo ni muhimu katika kuleta maendeleo ya wananchi.

Aliwaahidi wabunge 169 waliochangia na kuunga mkono hotuba ya rais na kuzungumzia maeneo mbalimbali waliyobainishwa, kwa kusema serikali itayazingatia na kuyaingiza kwenye mipango ya serikali na katika bajeti ya serikali.

Waziri Mkuu alisema michango ya wabunge itasaidia katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi 2020-2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo 2021/22-2025/26, ambao utawasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango Jumatatu katika mkutano huo.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wabunge pamoja na kutekeleza michango waliyotoa na kuishauriwa kuweka kwenye utekeleza mipango na vipaumbele vyake,” alisema.

Alisema Serikali itazingatia ahadi na maelekezo za Rais Magufuli, aliyotoa wakati wa kufungua bunge katika kupanga bajeti na mipango yake mbalimbali nchini, lakini kuibuliwa kwa hoja nyingi katika mijadala ni wazi kwamba hotuba hiyo imegusa maeneo mengi na yenye maslahi kwa wananchi. Alisema nchi inafanya juhudi kubwa katika kuandaa mipango inayowaletea wananchi maendeleo .

Kuhusu utoaji taarifa, Waziri Mkuu alirejea Hotuba ya Rais Magufuli aliyotoa Juni 4, 2018 wakati akizungua Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP II), kwa kuwataka viongozi hao kutumia nafasi zao kueleza mambo mengi mazuri ya kujivunia na yanayoendelea kutekelezwa kwani wananchi wanayo haki ya kupewa taarifa kadiri inavyoendelea.

Majaliwa alisisitiza kwamba viongozi wanatakiwa kwenda kusikiliza kero za wananchi na kwamba hicho ndicho kitakuwa kipimo cha kupima utendaji wao.

Chanzo: habarileo.co.tz