Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike kupeleka wataalamu wengi wa kilimo katika shamba la miwa la Mkulazi ili walisimamie kitaalamu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jioni ya Desemba 7, 2018 alipotembelea shamba la miwa Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro alipokuwa njiani kuelekea jijini Dodoma.
Amesema lengo la kuanzishwa shamba la miwa la Mkulazi ni jitihada za Serikali kuhakikisha mahitaji ya sukari nchini yanafikikia katika kiwango kinachohitajika.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga kuzalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na njia pekee ni kuboresha kilimo cha miwa, kujenga viwanda vitakavyozalisha sukari ya kutosha.
Amesema shamba hilo linaendeshwa kwa ubia kati ya NSSF na Jeshi la Magereza, kuagiza menejimenti mpya ya Mkulazi kuhakikisha shamba hilo linasimamiwa kikamilifu.
“Nataka shamba hili lisimamiwe kitaalamu, uzalishaji uwe wa kitaalamu na liwe mfano na mashamba mengine, tusishindwe na watu binafsi,” amesema.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watafute mashine nyingine zitakazotosha kumwagilia shamba hilo wakati wa kiangazi ili miwa isiharibike na iendelee kuwa ya kijani wakati wote.
Pia, amewataka wakuu wa wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro kuhakikisha wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuchangamkia fursa ya kilimo cha miwa.
Amesema Serikali imeanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa lengo la kuwasaidia wakulima wapate mitaji ili waongeze tija.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Jenistar Mhagama amesema shamba la Mkulazi II ni miongoni mwa mashamba mawili yanayomilikiwa na wabia wawili yaani NSSF na Jeshi la Magereza.
Amesema walikubaliana wao na Magereza wafanye kazi kwa kuongozwa na uzalendo, maadili ya utendaji wa kazi, uaminifu ili mwisho wa siku mradi huo uwe na tija na uweze kuwafikisha katika malengo yaliyokusudiwa.
Amesema wanaamini fedha zilizowekezwa kwenye mradi huo ambazo ni za wanachama zinatakiwa zirudishe faida kwa wanachama wenyewe na kujenga uchumi wa Taifa.