Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameitaka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inakuwa na ofisi zake katika kila mkoa nchini.
Majaliwa alitoa wito huo juzi alipotembelea banda la ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maonyesho ya wiki ya sheria yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere 'Square' Jijini Dodoma.
"Kwa kuwa sasa mna muundo mpya na majukumu yenu yameongezeka yakiwamo ya uratibu na utoaji wa ushauri wa kisheria, itakuwa vema kuwa na ofisi kila mkoa ili wananchi wasisafiri umbali mrefu kwenda kutafuta au kuomba ushauri wa jambo la kisheria," alisema.
Waziri Mkuu alisema anaamini baada ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuundwa upya inakuwa na nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa tija.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, kuhusu majukumu ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Said Nzori alisema baada ya mabadiliko ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ofisi hiyo imekuwa na divisheni za kisheria tatu.