Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa ataja siri ya mafanikio kiwango cha ufaulu kuongezeka

254a14f5a4d7701ea5c3124b0b6bc1e8 Majaliwa ataja siri ya mafanikio kiwango cha ufaulu kuongezeka

Sat, 10 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema kiwango cha ufaulu nchini kimeongezeka kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 iliyoielekeza serikali kutoa elimu ya msingi bila ada.

Alisema serikali ya CCM imetumia Sh trilioni 1.09 kugharamia elimu ya msingi bila ada kwa shule za msingi na sekondari na kuwa shule mpya za msingi 905 zimejengwa na sekondari 228 nchi nzima, pia shule kongwe 73 zimekarabatiwa pamoja na ujenzi wa mabweni mapya 253 na maabara 227.

Aliyasema hayo juzi wakati alipozungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika kata za Songe na Kwediboma wilayani Kilindi na kata ya Chanika wilayani Handeni, Tanga katika mikutano ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais John Magufuli.

Alisema kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza imeongezeka kutoka milioni moja mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa wanafunzi milioni 1.6.

Pia Serikali imefuta michango yote ya hovyo waliyokuwa wakitozwa wanafunzi ikiwemo ya kuchangia huduma ya maji na ulinzi.

Akizungumzia fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kugharamia elimumsingi bila ada katika halmashauri ya wilaya ya Kilindi, Majaliwa alisema jumla ya Sh bilioni 2.64 zilitolewa kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

Majaliwa alisema jumla ya Sh bilioni 1.82 zilitolewa na serikali kwa shule 22 za sekondari wilayani Kilindi kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa hule, hivyo aliwaomba wananchi wawachague viongozi wa CCM kwani wana mikakati mizuri ya kuwaletea maendeleo.

Aliwaeleza wakazi wa Handeni kwamba serikali yao itaendelea kuwatumikia na kuboresha huduma za jamii zikiwemo za elimu, maji na afya na kuwa serikali imetoa Sh milioni 83.8 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya hospitali ya wilaya ya Handeni.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM inalenga kuimarisha ubora wa elimu katika ngazi zote kwa kuzingatia falsafa ya kujitegemea yenye kuendana na mazingira ya nchi, hususan elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na katika kutimiza azma hiyo, Chama kitaielekeza serikali kushirikiana na sekta binafsi, asasi za kiraia zikiwemo taasisi za dini katika kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na ujuzi.

Chanzo: habarileo.co.tz