Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema wanafunzi 497 waliopo China kulikoibuka mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona wakiishiwa fedha watumiwe kwa njia ya mtandao ili waweze kujikimu.
Wanafunzi hao wanasoma katika vyuo vilivyopo mji wa Wuhan nchini humo ambao umeathirika zaidi na ugonjwa wa corona uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,500.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 16, 2020 katika kumbukumbu ya mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam iliyoandaliwa na Nida Textile Mills (T) Ltd na kufanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es Salaam.
Mji wa Wuhan umewekewa zuio hakuna mtu anayeruhusiwa kutoka wala kuingia, lengo likiwa ni kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo.
Majaliwa amesema kutokana na zuio hilo wakazi wote wa mji huo wakiwemo vijana wa Kitanzania wanapata huduma mbalimbali kupitia njia ya mtandao ukiwemo ununuzi wa bidhaa mbalimbali. “Hakuna usafiri hata wa umma unaofanya shughuli za kusafirisha watu katika mji wa Wuhan kila mmoja anatakiwa abakie katika makazi yake na Serikali ya China, uongozi wa vyuo unawatunza wanafunzi wote wakiwemo watanzania.” “Wachina wameimarisha utoaji huduma kwa njia ya mtandao hata kama mtu anataka kununua kitu ananunua kwa njia ya mtandao. Kama kijana ameishiwa basi atumiwe fedha kwa njia ya mtandao ili aweze kujikimu wakati huu wa zuio,” amesema Majaliwa.
Pia Soma
- Mifumo inavyowasumbua wananchi kwa kutoonana
- Maji Nyumba ya Mungu yaashiria hatari
- Serikali Tanzania yawaondoa hofu wafanyabiashara