Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aridhishwa kasi ya ujenzi wa SGR

E2845f71696bdb6bf7f086c614217b61.png Majaliwa aridhishwa kasi ya ujenzi wa SGR

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza kuridhishwa na kiwango na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliofikia asilimia 87 kwa kipande kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Alieleza kuridhika kwake baada ya kufanya ukaguzi jana wa ujenzi wa mradi huo na kusema serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli, anga, maji na barabara ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua aina ya usafiri wanaohitaji kuutumia na pia kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha biashara baina ya Tanzania na Mataifa mengine.

Waziri Mkuu ambaye alianza ziara hiyo kwa kukagua ujenzi wa jengo la stesheni ya Dar es Salaam ambalo linamuonekano wa madini ya Tanzanite, alisema ujenzi unaendelea vizuri na alimtaka mkandarasi akamilishe kwa wakati kwani watanzania wanasubiri kwa hamu.

Waziri Mkuu alisema watanzania waendelee kuiamini serikali yao kwa sababu imejipanga kuendelea kuimarisha ujenzi wa miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla na kuongeza kuwa huo ni utekelezaji wa maelekezo ya CCM iliyoyatoa kwa serikali yake.

Akiwa katika stesheni ya Ruvu mkoani Pwani, Waziri Mkuu alipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi yakiwemo ya wakulima kunyanyaswa na wafugaji kwa kuingiza mifugo katika mashamba yao hivyo kuwafanya wakose chakula.

Kufuatia malalamiko hayo Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo leo aende na wataalamu wake wakasikilize kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi, Atashasta Nditiye alisema mafanikio yanayoonekana katika mradi huo ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Alisema tayari mkandarasi anayejenga mradi huo kampuni ya Yapi Merkezi ameanza kufanya majaribio ya kupitisha treni za kihandisi katika baadhi ya vipande vya kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. “Mchakato wa manunuzi ya seti tano za mabehewa ya abiria unaendelea.”

Nditiye alisema licha ya ujenzi wa mradi wa SGR pia Shirika la Reli linatekeleza mradi wa uboreshaji wa Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka na maboresho hayo yamefikia asilimia 93 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Tabora na unatarajiwa kukamilia Februari 2021.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa alisema ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro unaendelea vizuri na umefikia asilimia 87 na kuongeza kuwa, “hadi sasa mkandarasi amelipwa jumla ya hati za malipo 34 sawa na Sh trilioni 1.7 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro. Mradi huo umetoa ajira zaidi ya 7, 400 Dar es Salaam-Morogoro.”

Alisema kazi ya ujenzi inayoendelea kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro ni pamoja na ujenzi wa daraja kubwa lenye urefu wa kilimita 2.56 na asilimia kwenye mabano majengo ya stesheni za Dar es Salaam (85), Pugu (99), Soga (100), Ruvu (95), Ngerengere (93), Morogoro (93), eneo la karakana na mizigo Kwala (73) na ujenzi wa madara 30 ambao umefikia (96).

“Ujenzi wa tuta la reli umefikia asiliamia 91, ujenzi wa mfumo wa mawasiliano ukijumlisha ujenzi wa minara 28 ya mawasiliano umefikia asilimia 43, ujenzi wa umeme wa msongo kv 220 upo asilimia 99, ujenzi wa vivuko 55 vikiwemo 20 vya juu, 17 vya chini na 13 vya wanyama na vitano vya makutano ya reli ya SGR na MGR, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 92,” alisema.

Chanzo: habarileo.co.tz