Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa apuliza kipenga sensa 2022

943d4053437d34c3a35e31895097342b.jpeg Majaliwa apuliza kipenga sensa 2022

Sun, 23 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amepuliza kipenga cha kuanza kikamilifu maandalizi ya sensa ya watu na makazi nchini itakayofanyika Agosti 28 mwakani kwa kuwataka Watanzania kutoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha utekelezaji wa kazi hiyo.

Sensa hiyo itafanyika baada ya miaka 10 tangu ilipofanyika mara ya mwisho mwaka 2012 ambapo Watanzania walikuwa milioni 44.9.

Makisio ya sasa yanaonesha kwamba katika sensa ya mwakani Watanzania wanatarajiwa kufikia kufikia milioni 64.

Akizindua Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi kwa Mwaka 2022, Waziri Mkuu, Majaliwa alisema, serikali imejiandaa na ipo tayari kufanya sensa hiyo muhimu kwa ajili ya kupanga mipango ya nchi na programu ilizoridhia za kikanda na kimataifa.

Alisema uzinduzi wa kitabu hicho unaashiria kupuliza kipenga cha kuanza kikamilifu maandalizi ya sensa kwa kasi na kufanya sensa ya majaribio Agosti 29, mwaka huu.

Alisema dhamira ya Serikali la Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha sensa inafanyika kuanzia na maandalizi kwa kuhakikisha fedha, vifaa yakiwamo magari 10 na vishikwambi vinapatikana kusaidia kufanikisha sensa hiyo kwa ufanisi mkubwa.

“Serikali ya Awamu ya Sita ya Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati ya kufanikisha sensa hiyo ili kupata kesho bora yenye takwimu zilizo sahihi zaidi,” alisema.

Sensa hiyo ambayo kwa asilimia 95 itagharimiwa na serikali tofauti na ya 2012 ambayo serikali ilichangia asilimia 90, itatumika kutathimini utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/17-2020/21), Dira ya Maendeleo (2025), Mpango wa Kimataifa wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (2030) na Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki 2050 na Agenda ya Maendeleo ya Afrika 2063.

Waziri Mkuu aliwataka wadau wa maendeleo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar katika kuhakikisha inafanikisha kufanya maandalizi ya sensa hiyo na kukamilisha.

Aliwataka wadau hao wa maendeleo kusaidia kwa hali na mali, fedha na vitendea kazi katika kufanya maandalizi ya sensa ambayo si ya Tanzania pekee, bali ni ajenda ya kimataifa katika kuhakikisha inafanyika kwa ajili ya kupanga maendeleo ya nchi hiyo na takwimu zake kutumika na wadau hao.

Majaliwa alisema katika kufanikisha sensa hizo, kamati ya kitaifa ambayo yeye ni Mwenyekiti wake, kamati za mikoa, za wilaya na nyingine zitakazoundwa, zinatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano katika kuhakikisha elimu ya sensa inawafikia wananchi ili kujiandaa kwa sensa hiyo.

Pia aliwataka watalaamu watakaohusika katika kukusanya takwimu katika usiku wa kuamkia Agosti 28, mwakani, wahakikishe wanachukua taarifa mbalimbali za wageni wote watakaolala nchini iwe hata kwenye nyumba za wageni kupata hesabu kamili.

Pia aliwaagiza viongozi wa mikoa, wilaya, kata na vijiji, mitaa pamoja vitongoji wanapofanya ziara kwa wananchi wao kuifanya ajenda ya sensa kuwa ya kudumu kwa kuelimisha wananchi umuhimu wakekuondoa imani potofu za watu wanaodai sensa hizo zina madhara.

Waziri Mkuu aliwataka wananchi kutoa ushirikia-

no kwa watalaamu wa takwimu watakaopita katika maeneo yao ya vitongoji na mitaa kuwapa taarifa zote wanazohitaji katika kuhakikisha kukamilisha suala la kuhesabu watu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah, alisema wana uhakika sensa ya 2022 itafanyika vizuri zaidi kutokana na ofisi zote mbili ya Bara na Zanzibar kujiandaa na kuwa na watalaamuwa kutosha.

Abdallah ambaye ni Mwenyekiti Mwenza wa Sensa ya mwakani alisema, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ameridhia kufanyika kwa sensa hiyo kutokana na umuhimu wake katika kupanga mipango ya nchi kwa maendeleo ya wananchi wake.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Yusufu Hamad Msauni alisema wizara yake itahakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga sera, mipango na programu mbalimbali.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango (SMZ) Jamali Kassim Ali, alisema kutokana na umuhimu wa sensa hivi sasa wanakimbizana kuhakikisha fedha zinapatikana ili kufanikisha jukumu hilo muhimu.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Jacqueline Mahon, alisema wadau wa maendeleo wataendelea kuisaidia Tanzania kwa kuipatia raslimali mbalimbali kuhakikisha inafanikiwa kufanya sensa hiyo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz