Lindi. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vyumba viwili vya madarasa vikiwa na madawati vyenye thamani ya Sh80milioni kutoka kwa Benki ya CRDB.
Alipokea madarasa hayo jana Jumatatu, Desemba 31, 2018 katika Shule ya Sekondari Kassim Majaliwa iliyopo Kata ya Nachingwea Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Waziri Mkuu ameushukuru uongozi wa benki hiyo kwa msaada huo kwa maelezo kuwa utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa madarasa unaoikabili wilaya hiyo.
Amezitaka taasisi nyingine ziige mfano wa benki hiyo kwa maelezo kuwa imekuwa bega kwa bega kuchangia shughuli za kimaendeleo nchini.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kassim Majaliwa kutumia vizuri madarasa hayo na kutunza mali zilizopo shuleni hapo.
Amebainisha kuwa ujenzi huo ni mradi uliobuniwa na wakazi wa kata ya Nachingwea ili kuwawezesha watoto wao kupata elimu katika eneo lililo karibu na makazi yao.
Amesema awali wanafunzi wa kata hiyo walikuwa wanatembea umbali mrefu hadi Shule ya Sekondari ya Ruangwa jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kwao.
“Nawaomba wananchi wenzangu tuendelee kushirikiana katika kuibua na kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maendeleo kwenye kata yetu ya Nachingwea,” amesema.
Waziri Mkuu pia aliahidi kukabidhi kompyuta 20 kwa shule za sekondari tano ambazo ni Kassim Majaliwa, Likunja, Mnacho, Hawa Mchopa na Ruangwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema benki yao inathamini elimu na imekuwa ikirudisha kwa jamii faida wanayoipata kwa kuchangia shughuli za maendeleo.
Amesema mbali na msaada huo wa vyumba viwili vya madarasa na madawati yake, pia aliahidi kutoa Sh20milioni ili zitumike kununulia madawati yatakayosaidia kupunguza changamoto ya madawati wilayani Ruangwa.