Kakonko. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, amepiga marufuku wananchi wanaoishi mikoa ya pembezoni mwa nchi ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuacha mara moja kuingiza vibarua wa kulima mashamba nchini bila ya utaratibu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Februari 19, 2019 wakati akizungumza na wananchi katika stendi ya mabasi iliyopo wilayani Kakonko mkoani hapa.
Amesema kuingiza vibarua kutoka nchi jirani ni chanzo cha kuongezeka kwa uhalifu nchini na kuongeza kuwa kama mwananchi atahitaji vibarua wa kulima shamba lake aende kwa mkuu wa mkoa akajiandikishe na Serikali itawafata vibarua hao kwa utaratibu wa kiserikali.
"Mmekuwa mkiagiza vibarua wa kuwalimia mashamba yenu si vibaya lakini lazima mfate utaratibu wa kiserikali kwani kuna wengine wanawaleta lakini hawawalipi stahiki zao mwisho wa siku wanasambaa nchini na kusababisha kuongezeka kwa uhalifu na silaha za kivita, "amesema Waziri Mkuu.
Amesema kwa wale wanaoingia nchini kwa kufuata taratibu na sheria za kuvuka mpaka hawataruhusiwa kuingia nchini na silaha ya aina yoyote na atakayekiuka hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Ameitaka kamati ya ulinzi na usalama mkoa kuhakikisha swala hilo linaangaliwa na kufanyiwa kazi kwa karibu na umakini zaidi kwa ajili ya maslahi ya nchi zote mbili.
Wakati huo huo Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi katika jengo la halmashauri ya wilaya ya Kakonko lenye vyumba 136 ambalo hadi kukamilika litagharimu Sh4 bilioni.