Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa apiga marufuku ujenzi wa viwanda maeneo ya shule

97927 Pic+majaliwa Majaliwa apiga marufuku ujenzi wa viwanda maeneo ya shule

Wed, 4 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepiga marufuku shughuli zisizohusiana na taaluma kama ujenzi wa viwanda katika maeneo ya shule ili kutoa fursa kwa wanafunzi kuwa kwenye mazingira mazuri ya kujifunzia.

“Sheria inakataza kuweka matumizi yoyote yasiyokuwa ya kitaaluma katika maeneo ya shule kwani yanasababisha kelele hivyo wanafunzi kushindwa kusoma vizuri,” amesema.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni Jumanne  Machi 3, 2020 baada ya kupokea malalamiko ya wazazi kuhusu eneo la shule ya msingi Mshikamano iliyoko Halmashauri ya Mji Handeni kuuzwa kwa mfanyabiashara ambaye amefungua karakana ya kutengeneza magari.

Kufuatia hali hiyo, Majaliwa ameuagiza uongozi wa halmashauri hiyo ukazungumze na mfanyabiashara huyo  ili  aondoe karakana katika eneo hilo na kumtafutia eneo mbadala kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na eneo hilo libaki kwa ajili ya masuala ya kitaaluma.

Pia, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni upange matumizi bora ya ardhi kwa kuainisha maeneo ya makazi, biashara, viwanda na huduma za kijamii ili kuepuka mji huo kujengwa bila ya mpangilio.

Walimu wenye mahusiano na wanafunzi

Pia Soma

Advertisement
Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuwafikisha kwenye vyombo vya dola walimu watakaobainika kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.

 “Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike, ukimpa mimba, ukimchumbia au kumuoa adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela,” amesema.

Akizungumzia kuhusu uwepo wa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara ya viongozi wa kitaifa, Waziri Mkuu amesema kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa Halmashauri hawawatembelei wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekani wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” amesema.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

 “Serikali hii haimlindi mfanyakazi mbadhirifu, mwizi na asiyefanya kazi kwa weledi au anayebagua wananchi eti kwa uwezo wake wa kifedha au rangi au dini yake au chama chake. Hivi vitu havipo katika Serikali kila mwananchi aliyeko Nzega anatakiwa kuhudumiwa,” amesisitiza.

Chanzo: mwananchi.co.tz