Dodoma. Waziri Mkuu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea leseni ya usajili wa chaneli ya utalii ya Tanzania Safari ambayo itaiwezesha kuoneshwa kwa umma bila ya malipo yoyote na wamiliki wa visimbusi.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu leo Jumatano Januari 16, 2019 inaeleza kuwa makabidhiano hayo yamefanyika leo katika kikao kilichoitishwa na Majaliwa kwa lengo la kutaka kupokea mrejesho kutoka kwa wajumbe wa Kamati Maalum ya kusimamia uboreshaji wa Chaneli ya Utalii.
Akikabidhi leseni hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Rioba amesema kukamilika kwa usajili huo kumeiwezesha chaneli hiyo ianze kuonekana kwenye kisimbusi cha Azam namba 109.
Amesema kamati hiyo iliyoundwa Desemba 21, 2018 na inajumuisha wajumbe kutoka taasisi ambata za maliasili na utalii kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
“Baada ya kupata leseni sasa hivi tunaonekana kwenye kisimbusi cha Azam chaneli namba 109 na pia kwenye intelsat ambako tutaweza kuonekana kwenye nchi zote barani Afrika, sehemu kubwa ya bara la Ulaya na Uarabuni,” amesema.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Meja Jenerali mstaafu, Hamisi Semfuko amesema chaneli hiyo inaweza kuchangia upatikanaji wa matangazo kutoka kwa wamiliki wa hoteli, kampuni za kutoa huduma za utalii na wenye magari ya utalii.
Naye mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Dk Allan Kijazi amesema chaneli ya Tanzania Safari imekuja katika wakati muafaka kwa kuwa itaongeza juhudi za taasisi zao kutangaza vivutio vilivyopo nchini na hivyo kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa nje.