Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majaliwa aonya watumishi vikwazo kwa wawekezaji

D9dc4b9cd77d1a02491f5c63b7a5616d Majaliwa aonya watumishi vikwazo kwa wawekezaji

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Iringa ,huku akiwataka watumishi wa umma wenye wajibu wa kuwasaidia wawekezaji kuacha kuwasumbua badala yake kuwasaidia wawekeze kwa urahisi.

Alisema kumekuwa na usumbufu usiokuwa wa lazima kwa wawekezaji wanaoupata kutoka kwa watanzania wenye mamlaka ya kutoa vibali vya uwekezaji hasa kushindwa kutumia busara katika utoaji wa huduma.

Alisema wapo baadhi ambao hata wakiwaelekeza wawekezaji mambo kadhaa wanayotakiwa kuyafuata na wawekezaji hao wakichelewa kidogo kuyatimiza, hutozwa faini wakati ingetakiwa kueleweshana na kuyamaliza.

Alisema serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha sera na mazingira ya uwekezaji hasa kwa kuhakikisha usalama wa wawekezaji wawapo nchini huku akiwataka wadau kutekeleza kile wanachotakiwa kukifanya katika kuimarisha uwekezaji.

Mwongozo wa uwekezaji Iringa umewekwa kwenye kitabu na unatoa taarifa za uwekezaji katika sekta mbalimbali mkoani humo kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi hasa sekta za kilimo, utalii, ufugaji, madini ya vito na ya ujenzi.

Akizungumzia mwongozo huo, Majaliwa alisema unaziwezesha taarifa za uwekezaji mkoani Iringa kufika mikoa yote nchini pamoja na nje ya nchi kwa urahisi zaidi.

Alisema, mwongozo huo ni utekelezwaji wa kivitendo wa sera ya uwekezaji ambayo Rais John Magufuli amekuwa akiitekeleza kivitendo hasa akihamasisha uanzishwaji wa viwanda sehemu mbalimbali za nchi.

Alisema serikali inatambua mchango wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kwamba ipo tayari kuendelea kuimarisha mazingira bora ya kibiashara na uwekezaji.

Alisema mwongozo huo uliopo katika kitabu na njia ya mtandao unaonesha na kutoa sababu za kwa nini wawekezaji wafike kuwekeza mkoani Iringa na kujadili vivutio vyake ikiwa katika ardhi na maji ya kutosha.

Alisema:”Nimependa namna ambavyo mmewaelezea wawekezaji sababu za kuja kuwekeza Iringa, ninaunga mkono sababu hizo kama vile uwepo wa maji na ardhi yenye rutuba, hali ya hewa ya kutosha na mimi pia ninakuja kuwekeza Iringa, “Pia Iringa hakuna shida ya nguvu kazi kwa kuwa ni eneo bora la kazi tangu miaka ya nyuma, watumishi wa kufanya kazi katika mashamba wapo wa kutosha ila hata jiografia yake nzuri kwa kuwa inapakana na mikoa mingi na Iringa ni pumulio la makao makuu ya nchi Dodoma.”

Alisema kuwa miundombinu ya barabara ni mizuri kwa kuwa barabara zote za kutoka na kuingia mkoani humo ni lami tupu hivyo kuwa rahisi kufanya biashara za kila aina na kila mkoa.

Aliongeza kuwa serikali inatoa Sh bilioni 41 kupanua ujenzi wa uwanja wa ndege Iringa ili kuziwezesha ndege za aina mbalimbali kutua mkoani humo kwa urahisi.

Aliongeza kuwa serikali inataka kuufanya mkoa huo kuwa wa kimkakati kwenye uwekezaji. Aliwataka wawekezaji kujitokeza zaidi kuwekeza kwenye mashamba ya miti, maparachichi na kuwa kuna mazao mengi ya kimkakati ambayo yataanzishwa Iringa kwa manufaa ya nchi.

Aliongeza kuwa serikali inazidi kuandaa mazingira bora zaidi ya uwekezaji ambapo mbali na kuwawezesha kufika kwenye maeneo ya uwekezaji lakini pia inasimamia nidhamu ya watumishi wa umma ambao wanasimamia uwekezaji hasa kuhakikisha hawawasumbui wawekezaji hao.

Alisema serikali imeondoa tozo 175 zilizokuwa kero kwa wawekezaji huku huduma za uwekezaji kwa sasa zikipatikana sehemu moja ili kuwasaidia wawekezaji kukamilisha mchakato wa uwekezaji kwa muda mfupi.

Alisema kuna vielelezo vingi vinavyoashiria kuwa uwekezaji umeleta tija nchini ambapo anatolea mfano wa mwenendo wa uchumi wa nchi kwa sasa kuwa Tanzania imeingia katika uchumi wa kati, pia imezuia mfumuko wa bei pia imeimarisha udhibiti wa mapato kuanzia kuyakusanya na kuyatumia.

Aliutaka uongozi wa Mkoa wa Iringa kuandika vitabu vya mwongozo huo wa uwekezaji kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha watanzania pia kuufahamu mwongozo huo kwa urahisi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alibainisha kuwa kitabu hicho kimehusisha maafisa kuanzia ngazi ya Kata, Halmashauri, Tarafa na Mkoani ili kutoa nafasi ya kila sehemu kuelezea kuhusiana na fursa za uwekezaji katika maeneo yao.

Alisema Mkoa huo umetenga maeneo ya kutosha ya uwekezaji katika sekta mbalimbali na kuwataka wadau pamoja na taasisi za serikali kujitokeza kutumia fursa za uwekezaji kwenye maeneo hayo.

Chanzo: habarileo.co.tz